TWIGA NA MWENDO WAKE WA MADAHA

 Emakulata Msafiri

Kulikuwa na mnyama mmoja mrefu sana mwenye shingo ndefu na miguu mirefu huyu si mwingine ila Twiga. Twiga alikuwa akiishi katika savana pana pamoja na wanyama wengine kama vile pundamilia, nyati, simba na chui.

Lakini kulikuwa na jambo moja la kipekee kumhusu Twiga mwendo wake wa madaha. Hakutembea kwa haraka wala hakukimbia ovyoovyo kama wanyama wengine. Alitembea kwa hatua ndefu, tulivu kana kwamba dunia nzima ilikuwa ikimsubiri. Wanyama wengine walimcheka.

"Twiga! Hebu ona mwendo wako huo wa kifalme. Unadhani wewe ni nani?" pundamilia alimtania.

"Huyo ni mtembea taratibu hadi mchana ufike usiku!" simba aliongeza kwa kejeli.

Lakini Twiga hakukasirika. Alitabasamu tu na kuendelea na safari yake akicheua majani ya mti wa mninga kwa starehe akiwa juu kabisa kuliko wote.


Siku moja jangwani kulitokea tatizo kubwa moto wa nyika. Moto huo uliwaka kwa kasi ukikimbia kwa nguvu kwa msaada wa upepo mkali. Wanyama wote walikimbia ovyo kila mmoja akijaribu kuokoa maisha yake. Ilikuwa vurugu tupu. Wanyama wakashindwa kuelewana kila mmoja akifuata njia yake wengine hata wakaingia shimoni au kupotea msituni.

Lakini yule Twiga kwa mwendo wake ule ule wa madaha alisimama juu ya kilima kidogo akaangalia kwa mbali akaona njia salama ya kutoroka. Kwa sauti yake ya upole lakini yenye mamlaka aliwaita wanyama:

 "Ndugu zangu msiende hovyo! Fuateni mimi. Kuna njia upande wa mashariki karibu na mto. Moto haujafika huko!"

Wanyama wakiwa wamechoka na wakiwa wamejaa hofu walimfuata Twiga. Hatua kwa hatua kwa utulivu Twiga aliwaongoza hadi mahali salama. Moto ulipopita wanyama wote walikuwa salama kwa sababu ya hekima na utulivu wa Twiga.

emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872


0/Post a Comment/Comments