SIRI YA EMMY NA CHUMBA CHA NDOTO

 

Emakulata Msafiri

Kulikuwa na msichana mmoja aitwaye Emmy mwenye miaka kumi. Emmy aliishi na bibi yake katika nyumba ya mbao iliyokuwa pembezoni mwa mji. Emmy alikuwa mtoto mchangamfu, mwenye akili nyingi lakini alikuwa mdadisi kupita kiasi. Aliuliza maswali kila wakati:

“Kwa nini mbingu ni ya buluu?” ,“Kwa nini saa inaenda mbele si nyuma?” “Kwa nini watu hukasirika?”

Siku moja akiwa anafagia chini ya kitanda cha bibi yake Emmy aligusa mbao moja ya sakafu na kusikia sauti ya “klik!” Alipoiangalia kwa karibu aligundua ilikuwa mlango wa siri!

Kwa tahadhari na hamu ya kujua akausukuma mlango huo taratibu. Alijikuta kwenye chumba kidogo cha giza kilichojaa vichorochoro na taa ndogo za kung’aa. Ukutani kulikuwa na maandishi:

"Karibu kwenye Chumba cha Ndoto hapa kila fikra huweza kuwa kweli.”

Mara moja chumba kilimpeleka kwenye tukio la maisha halisi. Alikuwa shuleni akimuona rafiki yake Nuru akiwa kimya na mwenye huzuni. Emmy alimsogelea na kumuuliza kwa upole:

 “Unaendelea vizuri Nuru?” Kwa mara ya kwanza Emmy alisikia sauti ya moyo wa mtu mwingine. Aliweza kuhisi huzuni ya Nuru na akamfariji.

Chumba kilimrudisha nyumbani na maandishi yakatokea ukutani tena:

“Fahamu: kuelewa watu ni zawadi ya mioyo iliyo wazi.”

Emmy alitoka kwenye chumba hicho akiwa mwenye hekima mpya. Alijua kuwa kuuliza maswali ni vizuri lakini kusikiliza mioyo ya wengine ni muhimu zaidi.

Na kila alipohitaji kujifunza zaidi Emmy alirudi kwenye Chumba cha Ndoto akiwa tayari kupokea somo jipya la maisha.

emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872


0/Post a Comment/Comments