SHUKURU KWA KILE ULICHONACHO

Emakulata Msafiri

Mwanakwetukids

Katika kijiji kidogo kilichozungukwa na mashamba ya kijani na mto mpana wenye maji ang’avu aliishi mbwa mmoja mjanja lakini mwenye pupa. Mbwa huyu aliitwa Boi. Boi alipenda sana nyama kuliko chakula kingine chochote.

Siku moja jua lilikuwa linawaka ndege wakiruka angani na upepo mwanana ukivuma. Boi alitembea shambani akitafuta kitu cha kula alipata kipanda kidogo cha nyama.

Safari ya nyumbani ilimpeleka kwenye daraja dogo la mbao lililokuwa limejengwa juu ya mto. Maji ya mto yalikuwa safi sana kiasi kwamba yalionesha kila kitu kama kioo. Alipofika katikati ya daraja Boi akaangalia chini. Mara akashangaa kuona mbwa mwingine akiwa na kipande kikubwa zaidi cha nyama mdomoni!


Boi hakujua kuwa kile alichokiona kilikuwa kivuli chake mwenyewe kilichoakisiwa na maji. Akafikiri "Mbwa huyu ana kipande kikubwa kuliko changu. Nikimnyang’anya nitakuwa na vipande viwili vya kula!”

Tamaa ikamjaa moyo. Bila kufikiri mara mbili alifungua mdomo wake ili kung’ata kile “kipande” cha nyama cha mbwa wa kwenye maji. Lakini punde tu alipofungua mdomo kipande cha nyama alichokuwa nacho kilianguka majini.

Maji ya mto yalikuwa na mkondo mkali. Kipande cha nyama kilipelekwa mbali sana kwa kasi, kikazama na kupotea machoni. Boi akajaribu kukimbia pembeni ya mto akijaribu kukifuata, lakini maji yalikuwa ya haraka mno.


Sasa Boi akabaki amesimama kwenye daraja hana chochote. Alijuta sana. “Laiti nisingetamani zaidi ya nilichokuwa nacho ningekuwa nimeshafika nyumbani nikiwa na chakula kizuri,” aliongea kwa huzuni.

Alirudi nyumbani akiwa na tumbo tupu na moyo mzito. Tangu siku hiyo Boi alijifunza somo muhimu: Usiwe na tamaa kupita kiasi la sivyo unaweza kupoteza hata kile kidogo ulichobarikiwa nacho.

 

 

emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872

 

 

 

 

0/Post a Comment/Comments