Emakulata Msafiri
Watoto ni viumbe wasiojiweza ambao hutegemea watu wazima kwa kila jambo maishani mwao. Miongoni mwa haki zao za msingi ni haki ya kupendwa ambayo ni ya asili kwa kila mtoto bila kujali rangi, dini, hali ya kiafya au mazingira alikozaliwa. Upendo ni msingi wa maisha ya mtoto na huchangia sana katika ukuaji wake wa kimwili, kiakili, kihisia na kimaadili.
Kupendwa ni kuhisi kuthaminiwa, kukubaliwa na kulindwa. Mtoto anapopendwa huishi kwa furaha hujenga kujiamini na huweza kukua akiwa na mtazamo mzuri kuhusu maisha. Upendo huwajengea watoto msingi wa kuwa watu wema waadilifu na wachangiaji wa maendeleo ya jamii yao.
Kupendwa hakumaanishi kumpa mtoto vitu vya thamani au kumtimizia kila anachotaka bali ni kumjali, kumsikiliza, kumtia moyo na kumhudumia kwa huruma na subira. Watoto hupaswa kupendwa nyumbani na wazazi wao shuleni na walimu wao pamoja na jamii nzima.
Haki ya kupendwa ni moja ya haki muhimu kwa mtoto. Mtoto anayepata upendo hukua katika misingi bora ya utu, huruma na heshima. Ili kuwa na jamii bora na yenye maadili mema tunapaswa kuanza kwa kuwapenda watoto wetu. Kila mtoto anastahili kupendwa si kwa sababu ya alichonacho bali kwa sababu yeye ni mtoto.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872


.jpeg)
Post a Comment