MIOYO YETU INAAKISIWA NA MATENDO YETU

 

Emakulata Msafiri

Mwanakwetukids

Katika msitu wa Furahia aliishi nyani mmoja mdogo aliyeitwa Koko. Koko alikuwa mchongezi sana alipenda kuwacheka wanyama wengine kuwadhalilisha na kusema maneno mabaya. Hakuwahi kufikiri kama anayosema yanawaumiza wengine.

Siku moja alipokuwa akirukaruka juu ya miti aliona kitu kiking’aa ardhini. Alishuka kwa haraka kumbe ni kioo kilichoanguka kutoka kwa msafara wa binadamu uliopita.

Koko hakuwa amewahi kuona kioo maishani mwake. Alipokiangalia akaona uso wake lakini kwa mshangao kioo hicho kilikuwa cha ajabu! Badala ya kumuonesha uso wake wa kawaida kilimuonesha suraya mnyama mkali mwenye hasira na macho ya chuki.

Koko akashtuka akakimbia. Lakini kila alipojaribu kuangalia tena uso ule ule wa kutisha ulikuwa unamwangalia.

Aliamua kwenda kwa Bundi mnyama mwenye hekima msituni. Bundi akamsikiliza kwa utulivu na kisha akasema:

 "Kioo hicho kinaonesha si uso wako wa nje tu bali moyo wako wa ndani. Kama umejaa chuki na dharau ndivyo utakavyoonekana."

Koko alinyamaza. Kwa mara ya kwanza alitafakari matendo yake. Alikumbuka jinsi alivyomcheka Kobe kwa kuwa mtembeaji wa polepole, alivyomwita Paa "mwoga"na alivyowahi kusema Tembo ni "mnene sana".

Akasikitika.Kuanzia siku hiyo Koko akaanza kubadilika. Alianza kuwa mkarimu akaomba msamaha kwa wote aliowahi kuwaudhi na akajifunza kusema maneno ya upendo na kutia moyo.

Baada ya wiki chache aliporudi tena kuangalia kwenye kioo kwa mshangao wake akaona uso wake wa kweli msafi, mchangamfu na mwenye furaha.

emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872


0/Post a Comment/Comments