MADHARA YA VITU VYA SUKARI KWA WATOTO


Emakulata Msafiri 

Katika jamii ya sasa wazazi na walezi wengi wamezoea kuwapa watoto wao vitu vyenye sukari kama zawadi njia ya kuwafariji au hata kuwaonesha upendo. Vitu hivi ni kama pipi, soda, biskuti, peremende, chokoleti na vyakula vingine vyenye sukari nyingi.Tabia hii ina athari nyingi kwa afya na maendeleo ya mtoto. Insha hii itajadili kwa kina athari za kuwapa watoto vitu vyenye sukari nyingi.

Sukari nyingi huathiri afya ya meno ya watoto. Watoto wanaopenda sana pipi na soda hukumbwa mara kwa mara na matatizo ya kuoza kwa meno. Hali hii huwalazimu watoto wengi kwenda kwa madaktari wa meno mara kwa mara jambo ambalo linaweza kuepukika iwapo wazazi watawapa vyakula vyenye afya bora.

Matumizi ya sukari kupita kiasi husababisha ongezeko la uzito wa kupindukia au unene uliokithiri (obesity) kwa watoto. Vyakula vyenye sukari nyingi vina kalori nyingi lakini havina virutubisho vya maana. 

Watoto wanapokula vyakula hivi kwa wingi bila kufanya mazoezi ya kutosha husababisha mwili kuhifadhi mafuta mengi. Unene huweza kupelekea magonjwa mengine kama kisukari cha aina ya pili, shinikizo la damu na matatizo ya moyo hata kwa watoto wadogo.

Ni wazi kuwa kuwapa watoto vitu vyenye sukari nyingi huathiri afya yao maendeleo ya akili na tabia zao kwa ujumla. Wazazi na walezi wana jukumu kubwa la kuhakikisha watoto wao wanapata lishe bora na vyakula vyenye virutubisho badala ya kuzoea kuwapa zawadi za sukari. 


emakulatemsafiri@gmail.com 

0653903872

     

0/Post a Comment/Comments