FAIDA ZA NANASI KWA WATOTO


Emakulata Msafiri

Nanasi ni tunda tamu lenye ladha ya kipekee na rangi ya kuvutia. Tunda hili linapendwa na watu wengi hasa watoto kutokana na ladha yake tamu na ya kuchangamsha. Mbali na ladha yake nzuri nanasi lina faida nyingi kwa afya ya watoto na ni muhimu sana kujua kwa nini ni vizuri kuwalisha watoto nanasi mara kwa mara.

Nanasi lina vitamini C. Vitamini C husaidia kuimarisha kinga ya mwili kwa watoto. Watoto hukumbwa na magonjwa mara kwa mara kama mafua, kikohozi na homa. Kwa kula nanasi miili yao hupata nguvu ya kupambana na magonjwa hayo. Vitamini C pia husaidia kwenye uponaji wa majeraha madogomadogo ambayo watoto huweza kupata wanapocheza.

Faida nyingine ni kwamba nanasi lina kiwango kidogo cha kalori na husaidia kuweka uzito wa mtoto katika hali nzuri. Katika dunia ya sasa watoto wengi wanakumbwa na uzito kupita kiasi kutokana na kula vyakula visivyo na virutubisho bora. Nanasi ni chaguo bora kwa sababu ni tunda lisilo na mafuta na lina sukari asilia inayofaa kwa mwili.


Aidha nanasi lina maji mengi jambo ambalo husaidia kuzuia upungufu wa maji mwilini. Watoto wanahitaji maji ya kutosha ili miili yao ifanye kazi vizuri. Kwa kula nanasi wanapata maji pamoja na virutubisho muhimu kwa afya yao.

Nanasi si tunda la kula kwa ladha tu bali ni hazina ya afya kwa watoto. Likiwa sehemu ya lishe ya kila siku linaweza kusaidia watoto kukua kwa afya kuwa na kinga dhabiti na kuwa na nguvu za kucheza na kujifunza. Wazazi wote wanapaswa kuhakikisha kwamba watoto wao wanapata tunda hili mara kwa mara ili wawe na afya bora na maisha marefu.

emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872


0/Post a Comment/Comments