Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids
Tango ni mojawapo ya matunda yanayopatikana kwa urahisi katika maeneo mengi duniani hasa katika nchi za tropiki kama Kenya, Tanzania na Uganda. Ingawa wengi hulitumia kama mboga katika mapishi ya kila siku kwa mujibu wa sayansi ya mimea tango ni tunda kwa sababu hutokea kutoka kwenye ua na huwa na mbegu ndani.
Tunda la tango lina maji kwa kiasi kikubwa zaidi ya asilimia 90 ya tango ni maji. Hii husaidia sana kuhakikisha watoto wanapata unyevu wa kutosha mwilini hasa wakati wa joto au wanapocheza na kufanya shughuli nyingi. Maji haya huimarisha kazi mbalimbali za mwili kama usafirishaji wa virutubisho utoaji wa taka mwilini na udhibiti wa joto la mwili.
Tango lina virutubisho vingi muhimu kwa afya ya mtoto. Lina vitamini C ambayo huimarisha kinga ya mwili na kumsaidia mtoto kupambana na magonjwa ya mara kwa mara kama mafua na homa. Pia lina vitamini K inayosaidia kuganda kwa damu pale mtoto anapojeruhiwa. Aidha tango lina madini kama potasiamu na magnesiamu ambayo husaidia katika ukuaji wa mifupa na kazi ya moyo.
Mbali na hayo tunda hili lina viambato vinavyosaidia kuboresha ngozi na macho ya watoto. Ngozi ya mtoto huwa laini hivyo kula tango husaidia kuifanya iwe na afya njema. Pia virutubisho vilivyomo katika tango huimarisha uwezo wa kuona jambo ambalo ni muhimu sana kwa mtoto anayejifunza darasani.
Tunda la tango ni zawadi kubwa kutoka kwa maumbile ambayo hutoa faida nyingi kwa watoto. Huwasaidia kuwa na afya bora, kinga imara ya mwili, mmeng’enyo mzuri wa chakula na ngozi yenye mvuto. Wazazi na walezi wanapaswa kuwahamasisha watoto wao kulipenda na kulila tunda hili mara kwa mara kama sehemu ya lishe bora.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872
Post a Comment