Emakulata Msafiri
Katika kijiji cha Kijani, aliishi mtoto mmoja mcheshi sana aitwaye Tuntu. Alipenda kucheza, kukimbia, na kula peremende nyingi, lakini alikuwa na tabia moja isiyopendeza hakupenda kuoga wala kupiga mswaki!
Asubuhi mama yake alipomwambia:
“Tuntu, nenda ukaoge!”
Tuntu alijibu kwa kicheko:
“Aaah mama! Ngoja kwanza nimalize kutazama katuni!”
Na usiku alipokumbushwa kupiga mswaki, alijifanya yuko usingizini.
Siku moja, alipokuwa shuleni, alianza kushika tumbo.
“Aaah! Tumbo langu linauma!” Tuntu akalalamika.
Mwalimu wake, Mwalimu Amina, alimpeleka hospitali. Daktari alipochunguza, alimtazama kwa upole na kusema:
“Tuntu, unakula bila kunawa mikono, hupigi mswaki, na huogi vizuri. Tumbo lako linaumwa kwa sababu vijidudu vinafurahia uchafu wako.”
Tuntu alishtuka.
“Vijidudu? Wanafurahia mimi kuwa mchafu?”
Daktari alitabasamu:
“Ndiyo! Vijidudu hupenda mikono michafu, meno machafu, na miili isiyooshwa. Lakini ukiwa msafi kila siku, wanakukimbia!”
Kuanzia siku hiyo, Tuntu alianza Kuoga kila asubuhi na jioni, Kupiga mswaki mara mbili kwa siku, Kununua sabuni yake mwenyewe ya harufu nzuri na Kununua brashi mpya ya meno na kuitunza vizuri
Miezi miwili baadaye, aliitwa mbele ya darasa na mwalimu wake:
“Watoto, hebu mpigieni makofi Tuntu! Sasa ni mfano bora wa usafi!”
Tuntu alitabasamu, meno yake yaking’aa kama nyota!
emakulatemsafiri@gmail.com
Post a Comment