Emakulata Msafiri
Katika mji wa Iringa aliishi msichana mdogo aitwaye Sarah. Sarah alikuwa na ndoto kubwa ya kuwa mhandisi wa majengo kwa sababu alipenda kuona nyumba nzuri na barabara zikijengwa.
Kila siku alipokuwa shuleni walimu wake walimwambia “Ukisoma kwa bidii na kushikilia lengo lako unaweza kufanikisha ndoto zako.”
Lakini Sarah hakuwa na msimamo. Mara alipoona rafiki zake wakipiga muziki naye alisema
“Nataka kuwa mwanamuziki maarufu!”
Kesho yake aliposikia habari za marubani akasema “Sitaki tena kuwa mhandisi, nataka kuwa rubani.”
Kila siku alibadilisha ndoto na hakuwahi kumaliza alichokianza.
Siku moja alitembea mjini akiona majengo marefu na magari yakipita barabarani. Akaanza kuhisi huzuni kwa sababu hakujua tena ndoto yake ni ipi. Aliporudi nyumbani mama yake alimwambia kwa upole:
“Binti yangu malengo ni kama taa ya barabarani. Ukifuata mwanga wake unafika salama. Ukibadilisha njia kila mara utakosa kufika popote.”
Maneno haya yalimgusa sana Sarah. Akaamua kushikilia ndoto yake ya kwanza ya kuwa mhandisi wa majengo. Alianza kusoma kwa bidii kuandika ndoto zake na kuzifanyia kazi kila siku.
Miaka ilivyopita Sarah akawa mhandisi mashuhuri mjini na watu walimpongeza kwa kujifunza jambo moja muhimu:
“Malengo yakipotea ni kwa sababu hatuyashikilii. Tukiyashika kwa moyo na bidii hubadilika kuwa ukweli.”
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872


Post a Comment