MZINGA WA BIBI NYUKI

Emakulata Msafiri 

Katika kijiji kidogo cha Mwaseni, kulikuwa na msitu mzuri uliojaa maua ya kupendeza na nyuki waliorukaruka wakikusanya asali.

Kati ya nyuki wote, alikuwepo Bibi Nyuki nyuki mzee mwenye hekima, ambaye alikuwa kiongozi wa mzinga.

Bibi Nyuki alikuwa na desturi moja ya kipekee kila wiki, aliwaita nyuki wote na kuwaeleza hadithi moja ya maisha.

Siku moja, alimwita Nyuki mdogo aitwaye Toto.

“Toto, unajua nini maana ya kushirikiana?” Bibi Nyuki akauliza.

“Ni pale tunapofanya mambo kwa pamoja?” Toto akajibu kwa sauti ya kukisia.

“Ndiyo!” Bibi Nyuki akatabasamu. “Lakini si tu kufanya pamoja, bali kusaidiana kwa moyo mmoja.”

Toto akashangaa, “Kwa nini ni muhimu sana?”

Bibi Nyuki akaanza kusimulia:

“Miaka mingi iliyopita, mvua kubwa ilinyeshea mzinga wetu. Tulihitaji kuhamia haraka kwenye sehemu salama. Nyuki mmoja mmoja hakuweza kufanya lolote peke yake. Lakini tuliposhirikiana, tulijenga mzinga mpya kwa siku moja tu!”

Toto akatabasamu, akielewa sasa.

Siku iliyofuata, Toto alimsaidia nyuki mwenzake aliyekuwa amejeruhiwa kurudi kwenye mzinga. Bibi Nyuki aliona, akatabasamu tena.

“Umeelewa sasa maana ya kushirikiana, Toto. Wewe ni nyuki shupavu!”


emakulatemsafiri@gmail.com 


0/Post a Comment/Comments