MTOTO WA MACHOZI YA KIMYA

Emakulata Msafiri

Raju alikuwa mtoto wa miaka tisa aliyeishi katika mitaa iliyokua na kelele, vumbi na pilikapilika nyingi. Aliishi na mama yake tu.

Baba yake Raju aliachana na familia hiyo alipokuwa bado mchanga na tangu hapo maisha yakawa magumu.

Raju hakuwahi kuwa na viatu vizuri wala nguo mpya. Kila siku baada ya shule alikimbilia sokoni kusaidia kubeba mizigo ili apate hela ya kununua unga wa jioni. Hakuwahi kulia mbele za watu lakini ndani ya moyo wake kulikuwa na kilio cha kimya.

Siku moja akiwa shuleni alichelewa kuwasilisha kazi ya nyumbani kwa sababu alishinda soko zima bila muda wa kuandika. Mwalimu alimkaripia kwa hasira bila kujua maumivu yaliyokuwa moyoni mwake.

Aliporudi nyumbani alimkuta mama yake akiwa amepoteza fahamu kwa sababu ya uchovu kupita kiasi. Alilia sana usiku huo kwa sauti ya kimya machozi yakitiririka kimya kimya.

Lakini kilichomfanya Raju kuwa tofauti ni moyo wake wa kutokata tamaa. Alijua hakuwa na msaada mwingi lakini aliamua kuwa atabadilisha maisha yake kwa kusoma kwa bidii.

Alianza kusoma kila mara alipopata muda chini ya mwanga wa kandili au hata sokoni alipokuwa anangoja wateja. Aliwauliza walimu maswali alikaa na wanafunzi waliokuwa bora ili aelewe zaidi.

Miaka ilivyopita Raju alipita mitihani yake kwa alama za juu. Alipata ufadhili wa masomo na hatimaye akaenda chuo kikuu kusomea uhandisi.

Leo Raju ni mhandisi maarufu lakini bado hurejea sokoni na shuleni aliposoma kuwasaidia watoto wengine waliopitia maumivu kama yake.


emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872


0/Post a Comment/Comments