MTOTO ANAWEZA KUCHANGIA MAWAZO KATIKA FAMILIA

Emakulata Msafiri

Familia ni kundi la watu wanaoishi pamoja na kushirikiana kwa upendo na mshikamano. Ingawa mara nyingi wazazi huonekana kama watu wa kutoa maamuzi makubwa katika familia ni muhimu kutambua kwamba hata mtoto ana nafasi ya kuchangia mawazo yanayoweza kusaidia familia kuishi kwa amani, furaha na upendo.

Mtoto anaweza kutoa maoni au mawazo kuhusu mambo ya kila siku katika familia kama vile aina ya chakula cha kupikwa, mahali pa kwenda matembezi au shughuli za pamoja kama kusafisha nyumba.

Vilevile mtoto anaweza kutoa mawazo yanayosaidia kutatua migogoro ndani ya familia. Wakati mwingine wazazi au ndugu wanaweza wasielewane lakini mtoto anaweza kusema jambo la hekima litakalosaidia kutuliza hali hiyo.

Watoto wanaweza kuwa na mawazo ya kibunifu yanayosaidia familia kuendelea. Watoto wana fikra mpya na wanaweza kutoa mapendekezo kuhusu matumizi bora ya muda kusaidiana katika kazi za nyumbani au hata kusaidia watu wengine. Mtoto anapopendekeza kusaidia jirani au kutunza mazingira anakuwa anaonesha maadili mema ambayo familia inaweza kuyaendeleza.

Aidha mtoto akipewa nafasi ya kutoa mawazo anajifunza kuwa jasiri, mwenye kujiamini na mwenye kujali wengine. Watoto wanaosikilizwa hujenga tabia ya kupenda kueleza mawazo yao kwa heshima na nidhamu jambo ambalo huchangia kuwa na familia inayosikilizana na kuheshimiana.

Mtoto si mtu wa kupuuzwa au wa kuonekana hana mchango. Mawazo ya mtoto yanaweza kuwa na hekima kubwa na yanaweza kusaidia familia kuishi kwa amani na mafanikio. Ni jukumu la kila mzazi kuhakikisha mtoto anapewa nafasi ya kutoa mawazo yake kwa uhuru na kwa kupewa heshima anayostahili.

emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872


0/Post a Comment/Comments