Emakulata Msafiri
Kulikuwa na mti mkubwa sana uliokuwa umesimama katikati ya uwanja. Mti huu ulikuwa na matawi mapana, majani mengi ya kijani na kivuli kikubwa sana. Lakini tofauti na miti mingine haukuwahi kuzaa matunda.
Watoto wa kijiji walipenda kucheza chini ya mti huu. Na mara nyingine walilala chini ya kivuli chake wakisubiri jua kupungua. Lakini watu wengine waliusema mti huo vibaya.
“Mti huu unaonekana mzuri lakini hauna faida " alisema mama mmoja akiwa sokoni.
Siku moja mvua kubwa ilinyesha sana. Mto uliokuwa karibu na kijiji ukavunja kingo zake maji yakaanza kusambaa na nyumba nyingi zikaanza kujaa maji. Watu wakaanza kukimbia huku na kule wakitafuta pa kukimbilia.
Watoto wengi walikimbilia uwanjani na kujificha chini ya mti mkubwa usiozaa matunda. Kivuli chake kilikuwa imara sana na mizizi yake mikubwa ilizuia maji kuingia chini yake. Akina mama na baba wakaja kuwafuata watoto wao na kujificha hapo pia.
Mti ule ulilinda watu wote dhidi ya mvua na upepo mkali. Baada ya mvua kupungua watu wote walimwangalia mti kwa mshangao.
Mzee wa kijiji alisema kwa sauti: “Hatimaye tumejua thamani ya mti huu. Huenda hatoi matunda lakini ametulinda ametupatia kivuli na sasa ametusadia kupona mafuriko.”
Wote walishangilia na kusema,
“Kuanzia leo mti huu utaitwa ‘Mti wa Uzima!’”
Mti ulitabasamu kwa furaha. Alijua sasa kuwa kila mmoja ana umuhimu wake hata kama si kwa njia inayotarajiwa na wengine.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872
Post a Comment