Emakulata Msafiri
Hasira ni hisia ya kawaida ambayo kila binadamu huipata wakiwemo watoto. Hata hivyo, ni muhimu kujifunza jinsi ya kuizuia au kuidhibiti ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea kutokana na hasira zisizodhibitiwa. Mtoto anapojifunza kudhibiti hasira yake huweza kuishi kwa amani na kuelewana vyema na watu wengine.
Kwanza kabisamtoto anaweza kuzuia hasira kwa kutambua hisia zake. Watoto wengi huchanganyikiwa wanapokasirika kwa sababu hawajui wanachohisi au kwa nini wanahisi hivyo. Kwa kumfundisha mtoto kusema“Nimekasirika kwa sababu fulani” humsaidia kuelewa hali yake na kuanza kutafuta suluhisho badala ya kuonyesha hasira kwa kupiga kelele au kuharibu vitu.
Mbinu mbalimbali za kupunguza hasira ambazo mtoto anaweza kufundishwa. Kwa mfano mtoto anaweza kuvuta pumzi kwa utaratibu na kuhesabu hadi kumi kabla ya kuchukua hatua yoyote. Njia nyingine ni kujitenga na eneo la ugomvi kwa muda mfupi ili kupata utulivu.
Zaidi ya hayo ni muhimu kuweka mipaka na adhabu zenye kufundisha. Mtoto anapaswa kufahamu kwamba tabia kama kupiga kutukana au kuharibu mali si sahihi na kuna matokeo yake. Adhabu zinazolenga kumwelekeza si kumuumiza au kumdhalilisha hutoa nafasi kwa mtoto kujifunza kutokana na makosa.
Mwisho kabisa ni vyema kumpongeza mtoto anapojaribu kudhibiti hasira yake. Sifa au maneno ya kutia moyo huongeza hali ya kujiamini na kumhamasisha kuendelea kuwa mtulivu hata katika hali ngumu. Hili linaweza kumfanya mtoto awe na mwenendo mzuri shuleni, nyumbani na hata katika jamii kwa ujumla.
Mtoto ana uwezo mkubwa wa kuzuia hasira endapo atapewa mwongozo sahihi, msaada na mfano mzuri. Kudhibiti hasira si jambo la siku moja, bali ni safari ya kujifunza ambayo humsaidia mtoto kuwa mtu mwenye hekima, utulivu na maelewano katika maisha yake ya kila siku.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872
Post a Comment