JE, MTOTO MDOGO ANAWEZA KUWA NA MSONGO WA MAWAZO?

 

Emakulata Msafiri

Dhana iliyojengeka Katika jamii nyingi ni kwamba watoto hawana matatizo ya kimaisha, hivyo hawawezi kuwa na msongo wa mawazo. Wengi huamini kuwa hali hii huwapata watu wazima tu kutokana na majukumu ya kifamilia kiuchumi au kazi. Hata hivyo mtazamo huu si sahihi kabisa. Mtoto mdogo anaweza kukumbwa na msongo wa mawazo kwa sababu mbalimbali zinazomzunguka katika maisha yake ya kila siku.

matatizo ya kifamilia yanaweza kusababisha msongo wa mawazo kwa mtoto. Migogoro kati ya wazazi, kutengana kwa familia au hata kupoteza mzazi mmoja ni mambo yanayoumiza moyo wa mtoto. Watoto huhisi hofu, huzuni, au kutotambulika, hali ambayo huathiri afya yao ya akili. Kwa mfano mtoto anayeona wazazi wake wakigombana kila siku hujawa na hofu na huzuni ambayo huweza kugeuka kuwa msongo wa mawazo.

Pia mazingira ya shule pia ni chanzo kikubwa cha msongo kwa watoto. Mtoto anaposhindwa kuelewa masomo anapobughudhiwa (bullying) na wenzake au anapokosa msaada kutoka kwa walimu, huweza kujihisi hana maana. Kushindwa kwa mitihani mara kwa mara au shinikizo la kupata alama za juu pia huweza kumfanya mtoto ajione hana thamani hivyo kuathiri hali yake ya kiakili.

Ukosefu wa mahitaji ya msingi kama chakula, mavazi na makazi unaweza kuathiri sana akili ya mtoto. Watoto wanaokua katika mazingira ya umaskini hujihisi wanyonge na kukosa tumaini la maisha bora. Msongo wa mawazo kwa watoto katika hali hii hujionesha kwa njia kama vile kutokuwa na hamu ya kucheza kujitenga na wenzake au hata kulia mara kwa mara bila sababu ya moja kwa moja.

Ni kweli kwamba watoto wadogo wanaweza kuwa na msongo wa mawazo. Jamii inapaswa kubadili mtazamo na kuanza kuwasikiliza watoto kwa makini, kuwatia moyo na kuwasaidia kushughulikia changamoto zao. Malezi bora upendo wa familia na msaada kutoka kwa walimu ni nguzo muhimu katika kulinda afya ya akili ya mtoto. Mtoto mwenye furaha leo ni mtu mzima mwenye mafanikio kesho.



emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872


0/Post a Comment/Comments