Emakulata Msafiri
Waswahili wanasema "Samaki mkunje angali mbichi." Methali hii ina maana kwamba maadili, tabia na mwenendo wa mtoto hupaswa kujengwa tangu akiwa mdogo. Msingi huu wa makuzi huwekwa nyumbani.
Kila mtoto huzaliwa akiwa hana uelewa wa mema na mabaya. Ni kupitia kwa wazazi na walezi wake ambapo anaanza kujifunza jinsi ya kuishi na watu, jinsi ya kuheshimu, kusema kweli na kuwa mkarimu.
Wazazi wana jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa watoto wao wanapata malezi bora. Hili linajumuisha mahitaji ya kimwili kama chakula, mavazi, afya pamoja na mahitaji ya kiakili na kihisia kama upendo, ushauri na kuwa karibu na watoto.
Aidha wazazi ni kioo cha watoto wao. Mtoto huiga anachokiona kwa wazazi wake. Iwapo mzazi ni mlevi, mkorofi au mwongo kuna uwezekano mkubwa mtoto atakua akifanya mambo hayo hayo. Vivyo hivyo kama mzazi ni mnyenyekevu mwenye busara na mwenye hofu ya Mungu, basi mtoto naye atafuata njia hiyo.
Familia ni shule ya kwanza ya mtoto na ni pale anapowekwa msingi imara wa maisha. Wazazi na walezi wanapaswa kuchukua jukumu lao kwa umakini mkubwa kwani mtoto wa leo ndiye kiongozi wa kesho. Taifa imara hujengwa kwa familia imara.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872



Post a Comment