UTAPIAMLO KWA WATOTO

Emakulata Peter

Utapiamlo ni hali ya mwili kukosa virutubisho muhimu vinavyohitajika kwa ajili ya afya na ukuaji. Hali hii huwapata sana watoto wadogo hasa wale wanaotoka kwenye familia zenye kipato kidogo au wale wanaokosa kula chakula cha kutosha na chenye mchanganyiko wa virutubisho muhimu.

Watoto wanahitaji chakula bora kila siku ili miili yao iweze kukua vizuri wawe na nguvu na akili nzuri. Ikiwa hawapati chakula chenye protini, vitamini, madini na wanga kwa kiwango kinachofaa wanakuwa katika hatari ya kupata utapiamlo.

Kuna aina kuu mbili za utapiamlo zinazowapata watoto. Kwanza ni marasmus ambapo mtoto anakonda sana na mwili wake unakosa mafuta na misuli. Hali hii humfanya mtoto kuonekana dhaifu na mgonjwa. Aina ya pili ni kwashiorkor ambapo mtoto anakosa protini na mwili wake huvimba hasa miguu na uso. Nywele za mtoto hubadilika rangi na ngozi inaweza kupasuka.

Dalili nyingine za utapiamlo kwa watoto ni pamoja na udhaifu, kuchelewa kukua, kupungua uzito, kuwa na ngozi kavu na kushindwa kufanya shughuli za kila siku kama kucheza. Utapiamlo pia huathiri kinga ya mwili na kumfanya mtoto awe rahisi kushambuliwa na magonjwa kama kuharisha na nimonia.

Ili kuzuia utapiamlo wazazi na walezi wanashauriwa kumpatia mtoto chakula cha aina mbalimbali kama vyakula vya nafaka (ugali, wali) mboga za majani, matunda, maharage, samaki, nyama na mayai. Pia mtoto anapaswa kunywa maji safi na ya kutosha na kupewa huduma bora za afya.

 Utapiamlo ni tatizo kubwa linaloweza kuzuia ndoto za watoto na kuathiri maisha yao kwa ujumla. Ni jukumu letu sote kuhakikisha watoto wanapata lishe bora ili wawe na afya njema na kufikia ndoto zao za baadaye.


emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872


0/Post a Comment/Comments