SIRI YA KIJIJI CHA USIKU

Emakulata Msafiri

Wakati wa likizo ya shule watoto watatu Jeska, Ashuravna Ally walienda kumtembelea bibi yao kijijini. Kijiji kile kilikuwa tulivu sana mchana lakini wakazi walidai usiku kuna sauti za ajabu kutoka msituni.

Siku ya kwanza walipofika bibi aliwaonya:

"Msitoke nje baada ya saa mbili usiku. Kuna kiumbe kinachoitwa Mzee Mlalo. Anapita akitafuta watoto wanaocheza usiku ili awachukue."

Walipoambiwa hivyo Jeska na Ashura walicheka wakadhani bibi anawafanyia utani. Ally naye akasema, "Ah! Hao ni hadithi tu za kutisha!"

Lakini usiku ulipofika walipokuwa wakilala ghafla wakasikia mlio wa upepo mkali na vishindo vya hatua nje ya nyumba. Jeska akachungulia dirishani. Akaona kivuli kirefu cheusi chenye mikono mirefu na macho mekundu yakiwaka kama moto.

Ashura na Ally walitetemeka na kujifunika mashuka. Jeska akashindwa kusema neno.Mara mlango wa chumba ukagonga "tok tok tok..." kwa sauti ya ajabu.

"Fungueni mlango... najua kuna watoto wachangamfu humu ndani..." sauti nyembamba na baridi ikasema.

Watoto walipiga kelele kwa woga. Bibi akaamka haraka akachukua kopo dogo lililokuwa na chumvi takatifu. Akapiga kando ya mlango na ghafla kivuli kikapiga ukelele wa ajabu kisha kikayeyuka hewani kama moshi.

Baada ya tukio hilo Jeska, Ashura na Ally hawakuthubutu tena kutoka nje usiku. Waligundua kwamba hadithi za bibi ni za kweli na zina maana kubwa ya kuwalinda.



emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872


0/Post a Comment/Comments