SAFARI YA MABADILIKO YA CHIKU

 


Emakulata Msafiri

Katika mtaa wa Mabibo jijini Dar es Salaam aliishi msichana mdogo aitwaye Chiku. Chiku alikuwa na miaka saba tu na alikuwa anapenda sana kuvaa nguo nzuri, kula peremende na kutazama katuni.

Lakini Chiku alikuwa na tabia moja isiyopendeza alipenda kulia kila siku kwa sababu ndogo ndogo. Akikosa remote ya TV analia. Akiona kaka yake anakula kipande kikubwa cha keki analia. Akichelewa kuoga analia kwa sauti kubwa hadi majirani wamsikie!

Mama yake, Bi. Zainabu alijaribu kumfundisha mara nyingi. "Chiku mtoto mzuri hulia pale tu anapoumizwa au akiudhika kweli. Ukilia kila wakati hakuna atakayekuamini siku ukiwa na shida ya kweli."

Lakini Chiku hakubadilika.

Siku moja Chiku alikwenda kwenye duka la jirani kununua juice. Akiwa njiani mguu wake uligonga jiwe kwenye uwanja wa mawe akajikata na kuanguka chini. Alianza kulia kwa sauti:

"Mamaaaa! Nisaidieeeee!"

Watu waliokuwa jirani walimsikia lakini wakasema:

"Ah, huyo ni Chiku. Kila siku analia. Labda juice yake imeanguka tu."

Chiku aliendelea kulia lakini hakuna aliyemchukulia maanani. Aliketi chini kwa huzuni akijuta kwa nini kila siku alikuwa akilia ovyo.

Baada ya muda mama yake alipotoka nje kumtafuta alimkuta Chiku akiwa ameumia. Alimbeba na kumpeleka hospitali ndogo jirani.

Baada ya kupona Chiku alimkumbatia mama yake na kusema:

"Samahani mama. Kuanzia leo nitalia pale tu ninapoumizwa kweli."

Tangu siku hiyo Chiku alibadilika. Alijifunza kuvumilia, kusikiliza na kutumia maneno badala ya kilio kila wakati.


emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872


0/Post a Comment/Comments