Emakulata Msafiri
Kulikua na Wanyama wengi miongoni mwa wanyama hao aliishi Kobe mwenye akili nyingi na rafiki yake Sungura aliyependa mashindano. Kila siku Sungura alikuwa akijisifia “Mimi ni mwepesi mwenye akili na mchezaji bora wa kila kitu!”
Siku moja Sungura alimwambia Kobe:
“Kobe twende tukacheze mchezo wa bao. Najua nitakushinda haraka haraka!”
Kobe alitabasamu kwa upole na kusema:
“Sawa rafiki yangu, lakini kumbuka bao si mchezo wa kukimbia, ni wa kufikiri.”
Walikaa chini chini ya mti mkubwa wa mwembe, wakatandika bao lao, na wakaweka mbegu zao. Wanyama wengine kama Paka, Kuku na Mbuzi walikusanyika kuwatazama.
Sungura alianza kwa haraka akicheza bila kufikiri sana. Alikuwa akicheka na kusema “Nitamaliza huu mchezo kabla jua halijazama!”
Lakini Kobe alikuwa na utulivu. Kila alipopanga mbegu zake, alitulia na kufikiri kwa muda. Alijua kila shimo na kila hatua ya mchezo.
Kadri muda ulivyopita sungura alianza kuchanganyikiwa. Mbegu zake zilikuwa zinapungua, na Kobe alikuwa anaongeza zake kila upande. Hatimaye Kobe alishinda mchezo!
Wanyama wote walishangilia wakisema:
“Kobe ndiye mshindi wa bao!”
Sungura aliona aibu lakini Kobe alimshika mkono na kusema:
“Sungura usijali. Bao ni mchezo wa akili na uvumilivu. Ukijifunza kutulia, utakuwa bingwa pia.”
Tangu siku hiyo Sungura aliacha kujisifu akawa mnyenyekevu na alijifunza kucheza bao vizuri kutoka kwa rafiki yake Kobe.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872
Post a Comment