Na Emakulata Msafiri
Palikuwa na ndege mdogo aitwaye Chiku. Chiku aliishi juu ya mti mkubwa uliopo karibu na kijiji. Ndoto kubwa ya Chiku ilikuwa kuruka mbali sana, zaidi ya milima na mabonde, na kuona dunia yote.
Kila siku Chiku aliwatazama ndege wakubwa wakiruka mbali na alitamani sana kuwa kama wao. Marafiki zake walimcheka na kumwambia kuwa yeye ni mdogo sana na hawezi kufika mbali. Lakini Chiku hakukata tamaa. Kila siku alijitahidi kufanya mazoezi ya kuruka. Aliruka kutoka tawi moja hadi lingine, alipiga mabawa kwa nguvu na alijifunza kushinda upepo mkali.
Siku moja aliamua kujaribu kuruka mbali zaidi kuliko siku zote. Alianza kuruka juu sana, akapita juu ya miti, akaona mito, mashamba, na watu wakifanya kazi. Alifurahia sana kuona dunia tofauti na alijisikia mwenye furaha kubwa.
Akiwa angani, aliona kijiji kilichokuwa kinaungua moto. Alishuka haraka na kurudi kijijini kwake kuwaita ndege wengine. Wote kwa pamoja waliruka kwenda pale na kuanza kupeleka maji kwa midomo yao kuuzima moto. Baada ya muda moto ulizimwa. Watu wa kijiji kile walimshukuru Chiku kwa ujasiri na msaada wake. Kuanzia siku hiyo, Chiku hakuitwa tena mdogo, bali shujaa wa anga.
Hadithi hii inatufundisha kuwa tusikate tamaa kwenye ndoto zetu hata kama wengine wanatubeza. Ujasiri na bidii vinaweza kuleta mabadiliko makubwa na kusaidia wengine.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872
Post a Comment