MTOTO KUCHEUA

 

 Emakulata Msafiri

Mtoto kucheua ni jambo la kawaida linalotokea mara nyingi baada ya kunyonyeshwa au kula. Wazazi wengi hupata tabu kuelewa kwa nini watoto wao wanacheua lakini hii ni hali ya kawaida na yenye faida kwa afya ya mtoto.

Wakati mtoto anaponyonya au kunywa maziwa kwa chupa anameza pia hewa. Hewa hii huingia tumboni na kumfanya mtoto ajisikie kujaa au kupata maumivu. Ili kuondoa hewa hiyo mtoto hutumia njia ya kucheua. Kwa hiyo kucheua ni njia ya asili inayosaidia kuondoa gesi tumboni na kumfanya mtoto ajisikie vizuri.

Baada ya kunyonyesha wazazi wanashauriwa kumbeba mtoto wima kwa dakika chache ili kumsaidia acheue. Wengine hupiga mgongoni kwa upole kwa kutumia mkono. Mbinu hii husaidia gesi kutoka kwa urahisi na kuzuia mtoto kutapika au kulia kwa maumivu.

Kucheua kwa mtoto pia kuna faida nyingi. Husaidia kupunguza maumivu ya tumbo (colic), humrahisishia mtoto kulala vizuri na kumfanya awe na raha. Wazazi wanapaswa kujua kuwa mtoto kucheua si ugonjwa bali ni ishara kwamba mwili wake unafanya kazi vizuri.

Kwa kumalizia kucheua kwa mtoto ni jambo la muhimu sana kwa afya yake. Wazazi wanapaswa kuendelea kumsaidia mtoto acheue kila baada ya kunywa maziwa ili kumuepusha na matatizo ya tumbo na kumfanya awe na furaha.



emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872


0/Post a Comment/Comments