JE, MTOTO ANAYO HAKI YA KUTOA MAAMUZI?

 


Emakulata Msafiri

Katika jamii nyingi watoto huonekana kama viumbe wasio na sauti ambao hawapaswi kushiriki katika maamuzi yanayowahusu. Hata hivyo hoja hii inazidi kupingwa na wengi wanaoamini kuwa mtoto licha ya umri wake anapaswa kuwa na haki ya kutoa maamuzi hasa yale yanayohusiana moja kwa moja na maisha yake. Kwa kuzingatia mikataba ya kimataifa maadili ya kijamii na hali halisi ya makuzi ya watoto ni wazi kwamba mtoto anayo haki ya kutoa maamuzi kwa kiwango kinacholingana na umri na maendeleo yake ya kiakiliya

Kwa mujibu wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Mtoto (UNCRC) wa mwaka 1989, ibara ya 12 inasema: “Mtoto ana haki ya kutoa maoni yake katika masuala yanayomhusu na maoni hayo yaheshimiwe kulingana na umri na ukomavu wake.” Hii inamaanisha kuwa mtoto hapaswi kupuuzwa bali asikilizwe na kupewa nafasi ya kushiriki katika maamuzi muhimu ya maisha yake kama vile elimu, afya na makazi.

Pia kumruhusu mtoto kutoa maamuzi humjenga kisaikolojia na kijamii.Mtoto anayesikilizwa hujifunza kuwajibika, kuwa na kujiamini na kuelewa athari za maamuzi yake. Kwa mfano.mtoto anapoamua aina ya michezo ya kushiriki au shughuli za shule, hujenga uwezo wa kuchambua na kufanya maamuzi yenye maana. Hali hii humsaidia katika maisha ya baadaye kuwa raia mwenye uwezo wa kujieleza, kujitegemea, na kushirikiana na wengine katika jamii.

Kwa kuzingatia mikataba ya haki za binadamu maendeleo ya mtoto kisaikolojia, na hali ya kijamii ni wazi kuwa mtoto anayo haki ya kutoa maamuzi. Hata hivyo.haki hii inapaswa kutekelezwa kwa kuzingatia umri, ukomavu na usalama wa mtoto mwenyewe. Ni jukumu la jamii, serikali na wazazi kuhakikisha watoto wanasikilizwa na wanashirikishwa katika maamuzi yanayowahusu, ili kuwajenga kuwa watu wazima wenye maono na msimamo thabiti.

Marejeo(soma zaidi) :

United Nations. (1989). Convention on the Rights of the Child.  https://www.unicef.org/child-rights-convention/

emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872


0/Post a Comment/Comments