Na, Emakulata Msafiri
Watoto ni nguzo muhimu ya jamii yoyote ile. Ndiyo viongozi wa kesho na tegemeo la taifa katika maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa. Ili mtoto aweze kufikia ndoto zake na kusaidia familia pamoja na taifa kwa ujumla, ni lazima awe na afya njema. Afya ya mtoto ni jambo la msingi linalopaswa kupewa kipaumbele na kila mzazi, mlezi na jamii kwa ujumla.
Kwanza, mtoto mwenye afya njema hukua vizuri kimwili, kiakili na kihisia. Watoto wanaopata lishe bora chanjo kamili na huduma za afya kwa wakati huwa na uwezo mkubwa wa kujifunza wanapofika shuleni. Mtoto anapoumwa mara kwa mara, huathiriwa kiakili na kimwili na hata kushindwa kuhudhuria masomo ipasavyo. Hili huweza kusababisha kushindwa kwao kielimu na hata kuathiri mustakabali wao wa maisha ya baadaye.
Afya ya watoto huisaidia jamii kuwa na kizazi imara chenye uwezo wa kufanya kazi kwa bidii. Mtoto anapokua akiwa na afya huwa na nguvu akili timamu na maadili mema ambayo humwezesha kuwa raia mwema. Jamii yenye watoto wengi wenye afya ni jamii yenye uhakika wa kuwa na watu watakaoendeleza uchumi na ustawi wa taifa.
Aidha, huduma za afya kwa watoto hupunguza vifo vya watoto wachanga. Watoto wengi hupoteza maisha kwa sababu ya magonjwa yanayoweza kuzuilika kama kuhara homa ya mapafu, malaria na utapiamlo. Kwa kutoa chanjo ushauri nasaha kwa wazazi, na kuzingatia usafi wa mazingira tunaweza kupunguza sana tatizo hili.
Kwa upande mwingine, jamii inapaswa kuelimishwa juu ya umuhimu wa huduma za afya kwa watoto. Wazazi wanapaswa kuelewa umuhimu wa kunyonyesha kupeleka watoto kliniki kwa chanjo kuwapa lishe bora na kuhakikisha wanakua katika mazingira safi na salama. Serikali nayo inapaswa kutoa huduma bora za afya mashuleni na vijijini hasa kwa watoto wanaotoka familia zisizojiweza.
Afya ya mtoto ni msingi wa maendeleo ya mtu binafsi na taifa kwa ujumla. Kila mmoja wetu anayo nafasi ya kuhakikisha watoto wanapata huduma bora za afya ili waweze kukua na kuwa watu wazima wenye mchango mkubwa katika jamii. Mtoto mwenye afya ni taifa lenye matumaini.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872
Post a Comment