SIRI YA PORI LA MWEZI

 


Emakulata Msafiri

katika kijiji kidogo cha Milimani, aliishi mtoto mmoja jasiri aitwaye Susumila. Susumila alikuwa na miaka kumi tu, lakini alikuwa na moyo mkubwa na akili nyingi kuliko watoto wengine wa rika lake.

Kila mtu kijijini aliogopa kuingia kwenye Pori la Mwezi, mahali palipojaa miti mirefu na sauti za ajabu usiku. Wazee walikuwa wakisema kuwa ndani ya pori hilo kuna kiumbe cha ajabu ambaye huficha hazina ya kale iliyojaa dhahabu na mawe ya thamani. Lakini hakuna aliyewahi kuthibitisha hilo—ni hadithi tu iliyoenezwa kwa hofu.

Siku moja, mbuzi wa familia ya Susumila alipotea. Susumila aliamka alfajiri na kuchukua fimbo yake ya kutembelea. Akaaga mama yake na kusema:

"Lazima nimtafute mbuzi wetu. Nitakapoingia Pori la Mwezi, sitarudi bila yeye."

Mama yake alimtazama kwa wasiwasi, lakini akajua kuwa hawezi kumzuia Susumila aliyekuwa mjasiri kama simba.

Alipoingia ndani ya pori, mara moja alihisi upepo wa baridi na kusikia kelele za ajabu. Alitembea kwa tahadhari, macho yakiwa makini. Ghafla, mbele yake aliona jicho kubwa likiangaza kama taa. Alisimama, moyo ukidunda kwa kasi. Lakini, cha kushangaza, kilikuwa kiumbe wa ajabu aliyeonekana kama paka mkubwa wa rangi ya fedha.Susumila hakukimbia. Badala yake, alisalimia:

"Habari paka mkubwa. Samahani kama nimevunja amani yako. Natafuta mbuzi wangu."

Kiumbe huyo alimtazama kwa mshangao. Hakuna mtu aliyewahi kuzungumza naye kwa adabu kama hiyo. Kwa sauti ya upole, alisema:

 "Wengi huja hapa kwa tamaa ya hazina. Wewe ni wa tofauti. Mbuzi wako yupo salama, nimemhifadhi dhidi ya simba wa mwituni.

Kisha kiumbe huyo alimpeleka Susumila hadi kwenye pango salama. Mbuzi wake alikimbia kwa furaha, akimrukia Susumila.

"Kwa ujasiri wako na moyo wa upendo, utakuwa mlinzi mpya wa Pori la Mwezi," alisema kiumbe huyo.

"Lakini usiseme siri hii kwa yeyote. Watakuja kwa tamaa."

Susumila aliahidi kutunza siri hiyo. Alirudi kijijini akiwa shujaa, lakini hakumwambia mtu yeyote kuhusu alichokiona. Tangu siku hiyo, hakuna mbuzi aliyepotea tena, na Pori la Mwezi lilibaki kuwa mahali pa siri na usalama — likilindwa na mtoto jasiri aliyeitwa Susumila.

emakulatemsafiri@gml.com

0653903872


0/Post a Comment/Comments