Emakulata Msafiri
Kuna kijana mmoja anayeitwa Musa anaishi mjini Dodoma. Musa alikuwa anajulikana kama mtoto mcheshi lakini pia muongo mkubwa. Kila siku alikuwa anapenda kudanganya watu kwa kusema vitu vya uongo ili awaogope au awachekeshe.
Siku moja, Musa akiwa anaicheza mitaani alianza kupiga kelele, “Jamani! Jamani! Kuna mwizi ameiba simu pale!” Watu waliokuwa karibu akina mama, vijana, na wafanyabiashara walikimbia kwa haraka kwenda kumsaidia. Walipofika, hawakukuta mwizi yeyote. Musa akaanza kucheka, “Haha! Nilikuwa nawajaribu tu kuona kama mnakimbia kwa kasi!”
Watu walikasirika sana, wakamwambia, “Musa, usitudanganye tena. Hii tabia yako inaweza kuleta matatizo makubwa.” Lakini Musa hakusikia, akaendelea na mchezo wake wa uongo.
Baada ya siku chache Musa alipiga kelele tena, “Mwizi! Mwizi! Anaiba pochi ya mama mmoja!” Watu walitoka madukani na kwenye magari, wakakimbia kwenda kumuokoa. Walipofika, wakaona hakuna mwizi. Musa akacheka tena, “Haha! Mnaogopa sana!”
Siku moja, Musa alipokuwa akicheza karibu na stendi ya mabasi kweli aliona mwizi akijaribu kumvuta mama mmoja pochi. Musa akapiga kelele kwa nguvu, “Mwizi! Mwizi! Msaada!”
Lakini safari hii, hakuna mtu aliyemsikiliza. Wote walidhani anadanganya kama kawaida. Mwizi akafanikiwa kuiba na kukimbia.
Baada ya tukio hilo, Musa alihuzunika sana na kujifunza kuwa kusema uongo huondoa imani na kuharibu mahusiano na watu. Tangu siku hiyo, Musa akaamua kuwa mkweli kila wakati.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872
Post a Comment