Emakulata Msafiri
Kulikuwapo na nyani mcheshi sana aliyeitwa Nono, aliyekuwa akiishi katika msitu wa Furaha. Nono alikuwa maarufu kwa vichekesho vyake. Aliweza kuiga sauti za simba, kucheza kwa mikono miwili, na kuimba kama ndege wa porini. Wanyama wote walimpenda — hata fisi aliyekuwa mkali aliwahi kucheka hadi akaanguka chini!
Lakini siku moja, msitu ulipata ukame. Matunda yakakauka, mito ikapungua, na wanyama wakawa wakali na kimya. Hakuna aliyekuwa na hamu ya kucheka tena. Hali hiyo ilimhuzunisha sana Nono.
“Nitafanya kitu,” alisema kwa sauti ya matumaini. Alitengeneza jukwaa kwa matawi, akapamba mti mkubwa na maua, na kutangaza:
“Karibuni kwenye tamasha la vicheko!”
Wanyama walikusanyika kwa shaka. Lakini Nono aliporuka jukwaani, akaigiza fisi anayehubiri kama kasuku, msitu mzima ulilipuka kwa kicheko!
Simba alicheka mpaka machozi, twiga aliketi chini kwa mara ya kwanza, na hata kobe akatabasamu. Wanyama walisahau huzuni zao, na furaha ikarudi msituni.
Tangu siku hiyo, Nono alijulikana kama: Daktari wa Furaha wa Msitu wa Furaha.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872
Post a Comment