MTOTO MTIIFU ALIYEJENGA NDOTO ZAKE

  


Na, Emakulata Msafiri 

Palikuwa na kijiji kidogo kiitwacho Mwamgongo, kilichozungukwa na milima na miti ya kijani. Katika kijiji hicho aliishi mtoto mmoja aitwaye Samson. Samson alikuwa na miaka kumi na miwili, yatima wa baba, na aliishi na mama yake ambaye alikuwa mchuuzi wa mboga sokoni.

Tofauti na watoto wengine wa kijijini waliopenda michezo na utoro shuleni, Samson alikuwa na tabia ya kipekee. Kila asubuhi aliamka mapema, akasaidia mama yake kazi za nyumbani, kisha akaenda shuleni akiwa amevalia sare yake safi. Shuleni, Samson alikuwa msikivu kwa walimu, hakuwa na jeuri wala majibu mabaya. Hata walimu wake walimpenda na kumtegemea kama kiongozi wa darasa.

Siku moja, kijijini palitokea shindano la insha kuhusu "Mtoto Bora wa Kijiji." Watoto wote walialikwa kushiriki. Samson, kwa heshima na utiifu wake, aliamua kuandika kuhusu maisha ya mama yake na jinsi alivyomfundisha kuwa na nidhamu, kuwaheshimu watu na kufanya kazi kwa bidii.

Baada ya wiki moja, matokeo yalitangazwa. Samson aliibuka mshindi! Alipokea zawadi ya vitabu, daftari, na hata ufadhili wa shule hadi sekondari kutoka kwa mfadhili mmoja aliyeguswa na hadithi yake.

Wazee wa kijiji walimpongeza Samson, na wakamchagua kuwa kiongozi wa vijana wa kijiji. Alifanywa mfano wa kuigwa na watoto wengine. Samson aliendelea kuwa mtiifu, na baadaye alipata nafasi ya kusoma hadi chuo kikuu, ambako alisomea udaktari. Alirudi kijijini kuwatibu watu wake bila tamaa ya mali.




emakulatemsafiri@gmail.com 

0653903872

0/Post a Comment/Comments