MGENI WA SAA SITA USIKU

Na Emakulata Msafiri 

Usiku mmoja wa mvua kubwa, kijiji kidogo cha Mwanyenze kilizingirwa na giza totoro. Umeme ulikatika, na radi zilipiga kila baada ya dakika chache, zikipasua anga kama makelele ya pepo waliokasirika. Watu walikuwa ndani ya nyumba zao, wakijifunika mashuka wakisubiri mvua ipite.

Lakini kwa Bahati, msichana mdogo wa miaka kumi na mbili, usiku huu ulikuwa tofauti.

Alisikia mlango ukigongwa kwa nguvu. Mama yake alikuwa kitandani akiwa na homa kali, na baba yao alikuwa safarini. Kwa ujasiri uliochanganyika na hofu, Bahati alishika taa ya mafuta na kwenda kufungua mlango.

Alipofungua, kulikuwa na mtu mrefu sana aliyefunikwa kwa koti kubwa jeupe, uso wake haukuonekana vizuri kwa sababu ya kofia aliyovaa na mvua iliyomwagika usoni mwake. Alizungumza kwa sauti ya kukwaruza:

 “Nahitaji msaada. Tafadhali, naweza kuingia kwa dakika chache tu.”

Bahati alisita, lakini hakuweza kumkataa mgeni. Alimkaribisha ndani na kumketisha karibu na jiko. Mvua iliendelea kunyesha, na mgeni hakuongea sana. Bahati alihisi kitu kisicho cha kawaida, hasa kwa jinsi alivyomwangalia kwa macho ya kung'aa yaliyokuwa yanamulika kana kwamba si ya kawaida.

Baada ya muda, aliposogea kumpa chai, taa ya mafuta iliwaka mwangaza mkali – na hapo Bahati alimuona uso wa kweli wa mgeni. Hakukuwa na ngozi, hakukuwa na macho ya kawaida. Uso ulikuwa wa mfupa, kama fuvu la kichwa, lakini linacheka kimya kimya.

Bahati alipiga kelele kubwa sana, lakini sauti yake ikapotea ghafla kana kwamba imemezwa na giza. Mgeni alisimama taratibu, akasema:

“Umenisaidia leo. Nitakurudia... siku moja.”

Kisha akaondoka bila kufungua mlango — alipita ukutani kama kivuli kinachoyeyuka.

Asubuhi ilipofika, watu wa kijiji walikuta alama za miguu ya ajabu zikielekea kwenye nyumba ya Bahati miguu mikubwa yenye vidole vitatu tu. Bahati aliponea, lakini tangu siku hiyo, kila usiku wa mvua, mlango wake hugongwa saa ile ile, lakini huwa hafungui tena.




emakulatemsafiri@gmail.com 

0653903872

0/Post a Comment/Comments