Emakulata Msafiri
Kuna msemo wa Kiswahili unaosema "Usipomchapa fimbo mtoto, utamharibu." Msemo huu umetumika kwa muda mrefu na wazazi wengi kuhalalisha kupiga watoto kwa fimbo kama njia ya kuwaadhibu na kuwalea. Swali kubwa la kujiuliza ni je, kweli fimbo humlea mtoto au kuna njia bora zaidi?
Kwa upande mmoja, wapo wazazi na walezi wanaoamini kuwa fimbo inasaidia kumfundisha mtoto nidhamu na kumfanya aheshimu watu wazima. Wanadai kwamba mtoto anayeadhibiwa kwa fimbo huogopa kufanya makosa, na hivyo hukua akiwa na tabia njema. Kwa mfano, mtoto anaweza kuacha kusema uongo au kuiba kwa sababu anaogopa kuadhibiwa. Kwao, fimbo ni njia ya haraka ya kurekebisha makosa.
Hata hivyo, upande mwingine wa hoja unaonyesha madhara makubwa ya kutumia fimbo. Wataalamu wa saikolojia wanasema fimbo humfanya mtoto kuishi kwa woga na kupoteza kujiamini. Badala ya kujifunza tofauti ya mema na mabaya, mtoto anajifunza kuogopa tu. Pia, mtoto anaweza kukua akiwa na hasira na chuki moyoni, jambo linaloweza kuathiri maisha yake ya baadaye. Wengine wanaweza kuwa wakatili au wababe kwa wengine kwa sababu wamezoea vurugu wakiwa wadogo.
Mbali na hilo, fimbo inaweza kuharibu uhusiano kati ya mzazi na mtoto. Mtoto anaweza kuacha kuzungumza ukweli kwa mzazi kwa sababu anahisi hatasikilizwa bali ataadhibiwa tu. Kwa hiyo, njia bora ya kulea mtoto ni kuzungumza naye, kumueleza kosa lake, na kumsaidia kuelewa matokeo ya tabia mbaya. Mazungumzo na upendo vina nguvu zaidi kuliko fimbo.
Kwa kumalizia, fimbo si lazima katika malezi ya mtoto. Ingawa inaweza kuleta matokeo ya haraka, madhara yake ya muda mrefu ni makubwa. Ni vizuri wazazi na walezi wakajifunza kutumia njia nyingine za maelewano, mfano ushauri na kuhimiza nidhamu kwa upendo. Mtoto anayelelewa kwa upendo na kueleweshwa hukua akiwa na heshima, ujasiri, na kujiamini.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872
Post a Comment