FAIDA ZA UJI KWA WATOTO

Emakulata Msafiri

Uji ni mojawapo ya vyakula vya asili ambavyo vimekuwa vikihusishwa na lishe bora kwa watoto. Ni chakula kinachopikwa kwa kutumia nafaka kama vile mahindi, ulezi, mtama, au mchele. Wazazi wengi hupendelea kuwapa watoto wao uji, hasa wakati wa asubuhi, kwa sababu ya faida zake nyingi kiafya. Katika insha hii, nitazungumzia faida mbalimbali za uji kwa watoto

Uji hutoa nguvu kwa watoto. Nafaka zinazotumika kutengeneza uji huwa na wanga mwingi, ambao hubadilishwa kuwa nishati mwilini. Watoto huhitaji nguvu nyingi kwa ajili ya kucheza, kujifunza, na kufanya shughuli mbalimbali za kila siku. Kwa hivyo, mtoto anayekunywa uji kila siku huwa na nguvu na afya njema.

Pia husaidia katika kukuza na kujenga mwili wa mtoto. Baadhi ya nafaka kama vile ulezi na mtama zina protini ambazo husaidia katika ukuaji wa mwili. Pia, uji unaweza kuchanganywa na maziwa, karanga au mayai ili kuongeza virutubisho vinavyosaidia mtoto kukua haraka na kuwa na mwili imara

Uji huimarisha kinga ya mwili. Uji wenye virutubisho kama vitamini na madini husaidia mwili wa mtoto kupambana na magonjwa. Watoto wengi wanaonyweshwa uji wa asili uliochanganywa na vyakula vya virutubisho huwa na afya bora na huwa hawaumwi mara kwa mara. Hii ni muhimu sana hasa kwa watoto wa umri mdogo ambao kinga zao bado ni dhaifu.

Faida nyingine ni kuwa uji ni rahisi kumezwa. Watoto wadogo ambao bado hawajaanza kutafuna vizuri wanaweza kupewa uji kwa urahisi. Uji huwa mwepesi tumboni na husaidia mtoto kushiba haraka bila kusababisha matatizo ya mmeng’enyo wa chakula. Aidha, uji huboresha afya ya tumbo na husaidia mtoto kupata choo vizuri.

Mwisho, uji ni rahisi kupatikana na kuandaliwa. Karibu kila familia inaweza kumudu kupika uji kutokana na nafaka zinazopatikana kwa wingi mashambani au sokoni. Kwa gharama nafuu, mtoto anaweza kupata chakula chenye virutubisho vingi.


emakulatemsafiri@gmail.com

0653904872


0/Post a Comment/Comments