CHUMBA CHA KUMI NA TATU

 


Na Emakulata Msafiri

Timo alikuwa mtoto wa kipekee mdadisi kupita kawaida, mwenye akili ya kuchunguza kila kona ya maisha. Alipenda vitabu vya kale, ramani zilizochanika, na hadithi za majini, mizimu, na mambo yaliyosahaulika.

Kijijini kwao palikuwepo nyumba moja ya zamani, maarufu kwa jina la “Nyumba ya Muda Uliofungwa.”

Ilikuwa imefungwa kwa miaka mingi, lakini kila mtu kijijini alijua kuhusu chumba cha kumi na tatu. Kilijulikana kwa sauti zisizoeleweka, mwanga wa mshumaa unaowaka bila mtu yeyote ndani, na saa iliyoganda saa saba na dakika saba.

Siku moja, baada ya mvua kubwa kunyesha, Timo aliona mlango wa nyumba hiyo ukiwa wazi kidogo kama kwamba kitu kilikuwa kimeingia… au kutoka.

Bila kusita, akaingia ndani akiwa na tochi na daftari lake la “mambo yasiyoeleweka.” Alikumbuka onyo la bibi yake:

“Timo… usiguse mlango wa chumba cha kumi na tatu. Kuna muda haupaswi kuamshwa.”

Lakini Timo hakuogopa. Alifika kwenye mlango wa chumba hicho, uliokuwa umeandikwa kwa herufi za kuchovya damu:

“Usipoogopa, utaishi… lakini utasahau.”

Akausukuma mlango polepole. Ukaunguruma kwa sauti nzito kama mtu aliye na hasira. Ndani, kulikuwa na kiti cha mbao, kioo kikubwa kilichopasuka, na saa iliyoganda.

Tochi ya Timo ilianza kufifia.

Tik... tak...

Mara, sauti ya kina ilisikika kutoka kwenye kioo:

“Timo... hatimaye umefika. Umekuwa ukinitafuta kwenye vitabu. Sasa na mimi nakutafuta ndani yako.”

Kioo kikaangaza, na Timo akaona sura yake mwenyewe lakini si ile aliyozoea. Alikuwa mzee, macho yamezama, na sauti iliyojaa ukimya.

Ghafla, sakafu ikapasuka, na akaanguka kwenye giza lisilo na mwisho. Alipofumbua macho, alikuwa kijijini kwao tena, lakini kila kitu kilikuwa kimebadilika. Jua lilikuwa jeusi, watu walitembea nyuma mbele, na majina yao yalibadilika kila dakika.

Alikwenda kwa bibi yake, lakini bibi hakuwa na uso tena. Alimshika mkono na kusema:

“Timo... sasa wewe ni sehemu ya chumba. Kila anayekutazama ataona sura yao ya hofu. Huwezi kurudi. Unaweza tu kuzingatia kusahau.”

Timo alipiga kelele, akakimbia, na akajikuta tena kwenye chumba cha kumi na tatu. Saa ikagonga:

Saba na dakika saba.

Mara, kila kitu kilitulia. Mlango ulijifunga. Saa ikasimama.

Na tangu siku hiyo, hakuna aliyemwona Timo tena lakini kila mtu aliyewahi kuwa mdadisi sana, anasema usiku mmoja waliota chumba kilichojaa vioo na kwenye kila kioo, walijiona wenyewe wakiwa Timo.


emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872


0/Post a Comment/Comments