Emakulata Msafiri
Katika msitu mmoja mkubwa uliokuwa na wanyama wa kila aina, aliishi fisi mmoja aliyejulikana kwa uchoyo wake. Fisi huyu hakupenda kushirikiana na wanyama wenzake, na kila mara alipata chakula, alikificha ili ale peke yake.
Siku moja, msitu ulipatwa na ukame mkubwa. Vyanzo vya maji vilikauka na chakula kikawa kidogo sana. Wanyama walilazimika kusaidiana ili waweze kuishi. Lakini fisi mchoyo hakubadilika aliendelea kula kwa siri na kuwacheka wenzake waliokuwa na njaa.
Simba, mfalme wa msitu, alipoona hali hiyo, aliamua kuitisha mkutano wa dharura. Wanyama wote walikusanyika, isipokuwa fisi. Alikuwa kajificha akila mizoga aliyoweka akiba.
Simba alituma swala na nyani kumtafuta fisi. Walimkuta akijificha ndani ya pango lake akila kipande kikubwa cha nyama.
"Fisi," akasema nyani, "twende, wanyama wanakusubiri uje tusaidiane kupambana na njaa hii."
Fisi alikataa na kusema, "Mimi sina njaa, wala sihitaji kusaidiana nanyi. Nendeni mkahangaike huko."
Swala na nyani walirudi na kumweleza simba kilichotokea. Simba alikasirika sana lakini hakutaka kutumia nguvu. Badala yake, aliamua kufundisha fisi somo.
Usiku mmoja, simba aliwaita wanyama wote wakae kimya. Wakavamia pango la fisi na kuchukua akiba yake yote ya chakula, kisha wakaigawana kwa usawa.jj
Asubuhi fisi alipoamka, alikuta pango lake tupu. Alilia, akapiga kelele, lakini hakuna mnyama aliyemsikiliza.
Siku zilivyopita, fisi alianza kuona njaa. Alipoenda kuwaomba wenzake chakula, wengi walimkumbusha alivyowadharau.
Hatimaye, fisi alijifunza kuwa uchoyo hauleti faida. Akaomba msamaha kwa wanyama wote na kuahidi kushirikiana nao siku zote.
Tangu siku hiyo, fisi hakuwahi kuwa mchoyo tena. Msitu ukarudi kuwa mahali pa amani na ushirikiano.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872
Post a Comment