SIRI YA USHINDI WA CHAUPELE

Na, Emakulata Msafiri

Chaupele alikuwa mtoto wa miaka kumi na moja anayeishi kijijini Mwembe-Tayari. Kila jioni baada ya masomo, watoto wa kijiji walikusanyika chini ya mti mkubwa wa mkuyu kucheza bao. Ingawa Chaupele alipenda kuangalia, hakuwahi kushinda hata mara moja alipocheza. Alikatishwa tamaa mara nyingi, lakini hakuwahi kuacha kujifunza.

Siku moja, Babu Rashid, bingwa wa zamani wa bao, alipita karibu na mti huo na kuona watoto wakicheza. Alikaa kando na kumuita Chaupele. "Kijana, unaonekana una moyo wa kujifunza. Je, unataka nijifunze nawe siri za bao?" Chaupele alikubali kwa bashasha.

Kila jioni, Babu Rashid alifundisha Chaupele mbinu za kupanga kete, kusoma nia ya mpinzani, na kuwa na subira. Alimwambia, "Ushindi wa bao si nguvu ya mikono, bali akili na utulivu wa moyo."

Baada ya wiki mbili, mashindano ya bao ya watoto kijijini yalifanyika. Wote walishangazwa Chaupele alipoanza kuwashinda wachezaji mmoja baada ya mwingine. Aliwasiliana kwa heshima, alicheza kwa utulivu, na kila mara alipiga bao huku akitabasamu.

Hatimaye, Chaupele alifika fainali na kucheza dhidi ya Mosi, mtoto aliyekuwa akijigamba kuwa ndiye bora. Wote walikaa kimya. Kwa ustadi alioupata kwa babu Rashid, Chaupele alicheza kwa umakini na akashinda.

Watoto walimshangilia, na Mosi alimkumbatia Chaupele huku akisema, “Leo umenifundisha kuwa bao si mchezo wa kujivuna, bali wa busara.”

Tangu siku hiyo, Chaupele hakuwa tu bingwa wa bao, bali pia alikuwa mfano wa kuigwa kwa watoto wote wa kijijini.

 


emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872

 

 

 

0/Post a Comment/Comments