Na, Emakulata Msafiri
Palikuwa na mwewe mmoja aliyeishi juu ya mlima mrefu sana. Mwewe huyu alikuwa na mbawa kubwa na nguvu, macho makali yaliyoweza kuona mbali, na alijulikana kwa uwezo wake wa kuruka juu angani kwa mizunguko ya ajabu.
Siku moja, alipokuwa anaruka angani kutafuta chakula, aliangalia chini na kuona kitu kikiwa kinatetemeka ardhini. Aliporuka karibu, aligundua kuwa ni kifaranga mdogo wa kuku aliyekuwa amepotea kutoka kwa mama yake. Kulikuwa na tai waliokuwa wakizunguka karibu, wakitaka kumla.
Mwewe huyo akasikitika. Kwa huruma, alimchukua yule kifaranga na kumpeleka kwenye kiota chake juu ya mlima. Alimlinda, akamlisha, na kumlea kama mwanawe mwenyewe. Kila siku alimfundisha jinsi ya kupaa angani, jinsi ya kutumia mbawa zake, na jinsi ya kuwa jasiri.
Lakini kila walipokuwa wakijaribu kuruka pamoja, kifaranga alisema:
“Mimi siwezi kuruka kama wewe. Mimi ni kuku tu! Kuku huruka chini tu, si kama mwewe anayeruka juu sana.”
Mwewe alimtazama kwa huruma na kusema:
“Ndiyo, ulikuwa na kuku, lakini umelelewa kama mwewe. Mbawa zako ni za kuruka juu. Wewe unaweza, ila unaogopa. Usiogope kujaribu.”
Kifaranga alitikisa kichwa na kurudi chini, akaendelea kuchakura chakura kwenye ardhi kama kuku, akila punje na wadudu, huku wanyama wengine wakimcheka na kusema:
“Mbona unajifanya kama ndege wa porini ilhali wewe ni kuku tu?”
Miaka ikapita. Mwewe mzee alizeeka na hatimaye akafariki. Kifaranga sasa alikuwa mkubwa, lakini bado aliishi kama kuku wa kawaida. Siku moja, kulikuwa na upepo mkali sana uliovuma kutoka mlimani. Upepo huo ulimtupa hewani kwa ghafla.
Kwa hofu, alichapachapa mbawa zake kwa nguvu ili asianguke – na kwa mshangao wake, alianza kupaa! Alizidi kuchapua mbawa, akapaa juu zaidi, hadi akaona dunia yote ikionekana kuwa ndogo chini yake. Alikuwa ameruka juu kama mwewe halisi!
Ndipo alikumbuka yale yote aliyofundishwa na mwewe yule mzee – na kwa mara ya kwanza, alijua kuwa yeye hakuwa kuku wa kawaida. Alikuwa amezaliwa na uwezo mkubwa, lakini alikuwa ameogopa kuamini hilo.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872
Post a Comment