MCHEZO WA KIBANDASKY

 

Na, Emakulata Msafiri

Katika mtaa wa Wakulima, karibu na shule ya msingi, palikuwa na kibanda maarufu cha chakula kilichoitwa "Kwa Mama Kibandasky". Kibanda hicho kilimilikiwa na mama mmoja mchangamfu aliyependa kupika chakula kitamu kwa watoto wa shule. Kila siku aliamka mapema, akapika chapati, wali, na supu ya maharagwe iliyopendwa na kila mtoto aliyeonja.

Watoto wengi walimpenda Mama Kibandasky kwa sababu hakuwa mkali, na mara nyingine aliwapa watoto chakula hata kama hawakuwa na pesa. Lakini kulikuwa na mtoto mmoja aliyeitwa Tunu, ambaye hakujifunza kuwa mkweli. Kila siku alifika kibandani, alidai ana njaa na angeleta pesa kesho. Kila siku hiyo "kesho" haikufika.

Mama Kibandasky alianza kugundua kuwa Tunu alikuwa ana tabia ya kudanganya. Lakini badala ya kumkemea au kumfukuza, aliamua kumfundisha kwa njia ya upendo. Siku moja, aliamua kumpa Tunu jukumu la kusaidia kusafisha sahani kabla ya kula. Tunu, ingawa alisita, alikubali kufanya kazi hiyo. Alipoimaliza, alipewa chakula chake na kupewa sifa kwa kazi nzuri aliyofanya.

Baada ya siku hiyo, Tunu alibadilika. Kila alipokuwa hana pesa, aliuliza kama kuna kazi angeweza kusaidia kufanya badala ya kula bure. Alijifunza kuwa maisha yanahitaji juhudi, ukweli, na nidhamu. Alijifunza pia kuwa hata chakula cha mtaani kina heshima, na kuwa kila mtu anapaswa kuheshimu kazi ya wengine.

Watoto wengine waliomuona Tunu wakaanza kumwiga. Kibanda cha Mama Kibandasky kiligeuka kuwa si tu mahali pa chakula, bali mahali pa kujifunza maadili mema.

Katika maisha, si kila kitu kinapatikana kwa kuomba tu. Mtu anayejifunza kusema kweli, kufanya kazi, na kuwa na heshima kwa wengine hupata zaidi ya chakula – hupata tabia njema na upendo wa jamii.



emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872


0/Post a Comment/Comments