LISHE BORA KWA WATOTO

 


Na, Emakulata Msafiri

Lishe bora ni nguzo muhimu ya maisha ya binadamu, hasa katika hatua za awali za ukuaji wa mtoto. Watoto wanapokuwa katika umri mdogo, miili yao huwa katika mchakato wa kujengeka kwa haraka na hivyo huhitaji chakula chenye virutubishi vya kutosha ili kusaidia ukuaji wao wa kimwili, kiakili, na kihisia. Bila lishe bora, hata mafanikio ya kielimu na afya njema hayawezi kufikiwa kikamilifu.


Kwa kawaida, lishe bora hujumuisha mlo kamili wenye virutubishi kama vile protini, wanga, mafuta, vitamini, na madini. Vyakula vinavyotoa virutubishi hivi ni pamoja na maziwa, mayai, samaki, mboga za majani, matunda, nafaka kama vile mahindi na mchele, pamoja na jamii ya kunde kama maharagwe. Mtoto anayepata mlo huu kila siku hujengeka vyema, huwa na kinga imara ya mwili dhidi ya magonjwa, na akili yake hufanya kazi kwa ufanisi.

Hata hivyo, si watoto wote wanaopata fursa ya kula lishe bora. Katika maeneo mengi, hasa vijijini na sehemu zenye umasikini mkubwa, watoto hukumbwa na lishe duni. Athari za lishe duni ni nyingi na ni mbaya. Mtoto hupatwa na utapiamlo, hudumaa, hukosa nguvu za kucheza na kujifunza, na huwa katika hatari kubwa ya kushambuliwa na maradhi. Aidha, watoto hawa hupoteza fursa nyingi za mafanikio maishani kwa sababu miili na akili zao hazikukua vizuri katika hatua muhimu za ukuaji.

Wazazi na walezi wana jukumu kubwa la kuhakikisha watoto wao wanapata lishe bora. Hili linaweza kufanikishwa kwa kupanga mlo wa familia kwa umakini, kutumia vyakula vinavyopatikana kwa urahisi lakini vyenye virutubishi, na kuepuka kuwapa watoto vyakula vya haraka visivyo na faida kiafya. Viongozi wa jamii pia wanapaswa kuelimisha wazazi kuhusu umuhimu wa lishe bora, na serikali ifanye juhudi za kuhakikisha kila mtoto anapata chakula cha kutosha, hasa kupitia shule na vituo vya afya.



emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872


0/Post a Comment/Comments