Na, Emakulata Msafiri
Kulikuwa na kijiji kidogo kilichozungukwa na milima na misitu minene. Kijijini humo aliishi mvulana mmoja aitwaye Bahati. Bahati alikuwa mtoto wa pekee wa mama yake, lakini alikuwa maarufu kijijini kwa utundu wake. Alikuwa hashikiki – akipewa kazi ya kuchunga mbuzi, anawapeleka kwenye shamba la watu. Akikatazwa kwenda mtoni peke yake, kesho yake yuko kule tena akielea kwenye kipande cha miti kama jahazi.
Mama yake alimpenda sana lakini alihangaika sana na tabia yake. “Bahati, mwanangu, siku moja utajifunza kwa njia ngumu,” mama yake alimwambia mara nyingi.
Siku moja, kijiji kilipigwa na mvua kubwa iliyosababisha mafuriko. Wazazi waliwaonya watoto wao kutotoka nje. Lakini Bahati, kwa ukaidi wake, alitoka kimya kimya. Alitaka kuona jinsi mto ulivyofurika.
Bahati alijitahidi kuelea, lakini maji yalikuwa na nguvu sana. Kwa bahati nzuri, kijana mmoja aliyekuwa akipita karibu alimsikia akipiga kelele na kumsaidia kumtoa mtoni. Aliporudi nyumbani, mama yake alikuwa tayari ameanza kulia, akidhani amempoteza mwanawe.
Siku hiyo Bahati hakusema chochote. Alikaa kimya, akitafakari. Tangu siku hiyo, alianza kubadilika. Akawa msikivu zaidi, na alijifunza kuwa kusikiliza ni jambo la hekima.
Mtoto mtundu hujifunza kupitia matukio, lakini upendo na uvumilivu wa walezi unaweza kumsaidia kubadilika kuwa mtu bora.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872
Post a Comment