Na,Emakulata Msafiri
Maji ni uhai, lakini si kila maji ni salama kwa matumizi ya binadamu. Watoto wengi hupenda kucheza na maji, hasa baada ya mvua au wanapoona mabwawa madogo ya maji yaliyojaa mitaani. Hili ni jambo la kawaida katika maisha ya utotoni, lakini linapohusisha maji machafu, huleta hatari kubwa kwa afya ya mtoto na hata kwa jamii nzima.
Kuchezea maji machafu ni jambo linaloshuhudiwa sana katika maeneo ya mijini na vijijini, hasa mahali ambapo hakuna usimamizi mzuri wa usafi wa mazingira. Maji machafu huwa ni yale yenye uchafu kama tope, taka, kinyesi cha wanyama au hata kemikali kutoka viwandani. Watoto hushindwa kutambua hatari hizo na kuendelea kucheza kana kwamba ni mchezo wa kawaida.
Athari za kuchezea maji machafu ni nyingi. Kwanza, watoto hupata magonjwa ya tumbo kama kuhara na kipindupindu kutokana na kumeza au kugusana na maji yenye vimelea. Pili, huweza kupata minyoo, magonjwa ya ngozi kama upele na fangasi, na hata maambukizi ya macho. Kwa baadhi ya maeneo, ugonjwa wa kichocho ni tatizo kubwa linalosababishwa na kuchezea maji yaliyotuama kwa muda mrefu.Pia, kuchezea maji machafu huathiri maendeleo ya mtoto. Mtoto anapougua mara kwa mara, hukosa masomo, hupoteza nguvu za mwili, na hatimaye hupungua kiakili na kimwili. Hili linaathiri ndoto zake za baadae, na hata maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Sababu nyingine ya tatizo hili ni ukosefu wa elimu kwa wazazi na watoto kuhusu hatari ya maji machafu. Wengine huona kuwa ni jambo la kawaida mtoto kuogelea kwenye mitaro au mabwawa ya mvua, bila kujua madhara yake. Vilevile, ukosefu wa maeneo ya kuchezea salama huwafanya watoto kutumia sehemu hatarishi kama uwanja wa michezo.
Suluhisho la tatizo hili ni pamoja na kutoa elimu kwa wazazi na watoto kuhusu usafi na afya. Serikali inapaswa kuboresha miundombinu ya maji na kuhimiza ujenzi wa sehemu salama za kucheza kwa watoto. Viongozi wa jamii pia wanapaswa kusimamia usafi wa mazingira yao. Kwa upande wa shule, walimu wana jukumu la kuwafundisha wanafunzi umuhimu wa usafi wa mwili na mazingira.Kuchezea maji machafu ni hatari kubwa kwa watoto na ni jambo linalohitaji kuchukuliwa kwa uzito mkubwa. Tunapowalinda watoto dhidi ya madhara haya, tunajenga jamii bora, yenye afya na matumaini ya baadae. Watoto ni taifa la kesho, na ni jukumu letu sote kuhakikisha wanakua katika mazingira salama na yenye afya.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872
Post a Comment