Na Emakulata Msafiri
Katika kijiji kimoja tulivu karibu na msitu mkubwa, aliishi kasuku mwenye rangi za kuvutia aliyeitwa Ndumi. Ndumi alikuwa na manyoya ya kijani kibichi na buluu ang’avu. Kilichomtofautisha na ndege wengine ni kwamba alipenda sana kusikiliza wanadamu wakizungumza.
Siku moja, mtoto mdogo kutoka kijijini alipotea msituni. Alitembea kwa muda mrefu akitafuta njia ya kurudi nyumbani lakini hakuweza. Alipochoka, aliketi chini ya mti mkubwa na machozi yakaanza kumtiririka.
Kasuku Ndumi aliyekuwa juu ya mti huo alisikia kilio hicho. Akaruka hadi chini na kusema kwa sauti aliyojifunza kutoka kwa wanadamu:
“Usilie, nitakusaidia!”
Mtoto huyo alishangaa kusikia ndege akizungumza, lakini sauti ya Ndumi ilikuwa ya kirafiki. Ndumi alipaa juu ya mti na kuangalia kijiji kwa mbali. Akaona paa la nyumba moja liking’aa kwa jua.
“Nifuate!” kasuku alisema.
Ndumi aliruka kutoka tawi moja hadi jingine huku mtoto akimfuata. Hatimaye, walifika kijijini. Mtoto alipokutana na familia yake, wote walifurahi sana. Walimshukuru Ndumi kwa kumsaidia, wakampa matunda matamu kama zawadi.
Ndumi alipomaliza kula, alitazama kila mtu kisha akasema kwa sauti:
“Asante!”
Tangu siku hiyo, watoto wa kijijini walimpenda Ndumi sana. Alijulikana kama kasuku mwenye moyo wa upendo na heshima. Kila mtoto alijifunza kusema “asante” kama Ndumi.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872
Post a Comment