FAHAMU UGONJWA WA KICHWA MAJI KWA WATOTO

 


Na, Emakulata Msafiri

Kichwa maji ni ugonjwa hatari unaotokea pale ambapo majimaji yanayozunguka kwenye ubongo na uti wa mgongo (cerebrospinal fluid) yanapokusanyika kupita kiasi ndani ya kichwa. Ugonjwa huu hujulikana kwa jina la kitaalamu kama Hydrocephalus. Majimaji haya yanapokusanyika, huongeza presha kwenye ubongo na kusababisha kichwa kuvimba au kuongezeka kwa ukubwa, hasa kwa watoto wachanga ambao fuvu lao bado halijakomaa.

Watoto wengi walio na ugonjwa huu huonekana kuwa na vichwa vikubwa kuliko kawaida. Wengine hupata matatizo ya kuona, kushindwa kusimama au kutembea, na wakati mwingine huchelewa kuongea au kujifunza. Kwa watu wazima, kichwa maji kinaweza kuleta maumivu makali ya kichwa, kupoteza kumbukumbu, kutoweza kutembea vizuri na hata matatizo ya akili.

Sababu za kichwa maji ni nyingi. Kwa watoto wachanga, mara nyingi husababishwa na matatizo ya kuzaliwa nayo (maumbile ya kuzaliwa), maambukizi wakati wa ujauzito kama vile rubella au toxoplasmosis, au wakati mwingine kwa kuzaliwa njiti. Kwa watu wazima, ugonjwa huu unaweza kutokana na uvimbe kwenye ubongo, majeraha ya kichwa, au maambukizi kama meningitis.

Matibabu ya kichwa maji yapo, lakini ni ya kitaalamu na yanahitaji uangalizi wa karibu. Daktari bingwa wa upasuaji wa ubongo (neurosurgeon) huweza kuweka bomba maalum liitwalo shunt ambalo husaidia kuondoa maji hayo kutoka kwenye ubongo na kuyapeleka sehemu nyingine ya mwili, kama tumboni, ambako huweza kufyonzwa kwa kawaida.


Ugonjwa huu ukiwahi kugundulika, mtoto anaweza kuishi maisha ya kawaida baada ya matibabu. Lakini bila matibabu, kichwa maji huweza kuleta ulemavu wa kudumu au hata kusababisha kifo. Ni muhimu sana wazazi waangalie viashiria kama kichwa kuongezeka kwa kasi, macho kushuka chini (sunset eyes), mtoto kutonyonya vizuri, kulia sana au kulala kupita kiasi, na wachukue hatua haraka.



emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872 

 


0/Post a Comment/Comments