WATOTO WENYE ULEMAVU WA NGOZI

 


Na, Emakulata Msafiri 

Ulemavu wa ngozi, au albinism kwa jina la kitabibu, ni hali ya kuzaliwa ambayo husababisha ukosefu wa rangi ya kawaida ya ngozi, nywele, na macho kutokana na ukosefu wa kemikali iitwayo melanin mwilini. Hali hii ni ya kurithi na haambukizwi. Watoto wenye ulemavu huu wako katika jamii zetu na wanahitaji ulinzi, msaada na uelewa wa kipekee ili waweze kuishi kwa furaha kama watoto wengine.

Watoto wenye ulemavu wa ngozi hukumbana na changamoto nyingi zinazowakwamisha katika maisha yao ya kila siku. Kwanza kabisa ni suala la afya. Ngozi yao huwa nyepesi sana na huwafanya wawe katika hatari kubwa ya kupata magonjwa ya ngozi hasa saratani ya ngozi, kutokana na miale ya jua. Aidha, wengi wao hupata matatizo ya macho yanayowaathiri kimasomo na hata kimaisha. Kukosa mafuta maalum ya kuwalinda dhidi ya jua na vifaa vya kusaidia kuona ni tatizo kubwa.

Mbali na changamoto za kiafya, watoto hawa hukumbana pia na unyanyapaa na ubaguzi kutoka kwa jamii na hata familia zao. Wapo wanaodhulumiwa, kudharauliwa au hata kuachwa kusoma kwa sababu ya ulemavu wao wa ngozi. Mbaya zaidi, katika baadhi ya maeneo, watoto hawa huwa waathirika wa imani za kishirikina ambapo hujeruhiwa au hata kuuawa kwa imani kuwa viungo vyao vina nguvu za kichawi. Hii ni kinyume kabisa na haki za binadamu na utu wa mtoto.

Pamoja na changamoto hizo, watoto wenye ualbino wana haki sawa kama watoto wengine. Wana haki ya kuishi kwa usalama, kupata elimu, huduma bora za afya, na kushiriki kikamilifu katika maisha ya kijamii. Kwa bahati nzuri, serikali na mashirika mbalimbali yamekuwa yakijitahidi kuwalinda na kuwasaidia watoto hawa kwa kutoa elimu kwa jamii, kuwapa mafuta ya jua na vifaa vya macho, na kupiga vita mila potofu. 



Hata hivyo, bado kuna mengi yanayopaswa kufanywa. Familia ziwape upendo na kuwatetea watoto wenye albinism. Shule ziwape mazingira rafiki kwa masomo yao kwa kuzingatia mahitaji yao maalum. Serikali na taasisi binafsi ziongeze juhudi katika kampeni za elimu kwa jamii ili kuondoa kabisa unyanyapaa na dhuluma dhidi yao.

Watoto wenye ulemavu wa ngozi ni sehemu muhimu ya jamii. Wanayo haki ya kuishi maisha ya heshima, usalama na mafanikio kama watoto wengine. Ni wajibu wetu sote kama wazazi, walimu, viongozi na wananchi kwa jumla kuwalinda, kuwaunga mkono na kuwaheshimu. Dunia itakuwa mahali pazuri zaidi pale ambapo kila mtoto atathaminiwa bila kujali rangi, hali au tofauti yake.



emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872


0/Post a Comment/Comments