TENDA WEMA NENDA ZAKO

Na, Emakulata Msafiri

Hapo zamani za kale, palikuwa na kijiji kidogo kilichozungukwa na milima na misitu minene. Katika kijiji hicho aliishi mtoto mdogo aitwaye Amani. Amani alikuwa mchangamfu, mwenye bidii, na mwenye moyo wa huruma sana. Alipenda sana wanyama na kila siku alikuwa akiwasaidia kuku, mbwa, na hata paka waliopotea.

Siku moja, alipokuwa akitembea msituni kutafuta kuni kwa ajili ya mama yake, alisikia sauti ya kilio. Alifuata sauti hiyo hadi akamkuta mwana-mbwa mdogo aliyekuwa amejeruhiwa mguu. Amani alimchukua kwa upole, akamrudisha nyumbani, na kumtunza hadi akapona.

Baada ya siku kadhaa, Amani aliporudi tena msituni, alikutana na simba mkubwa! Alishtuka sana, lakini kabla hajakimbia, yule simba alisimama na kuanza kunusa-hewa. Ghafla, simba alimsogelea Amani, akamnusa, kisha akamramba mkono kwa upole. Amani alishangaa sana! Kumbe yule simba alikuwa ni rafiki wa yule mwana-mbwa aliyemsaidia.

Simba alitambua wema wa Amani kupitia harufu ya mwana-mbwa. Tangu siku hiyo, Amani alipata ulinzi wa ajabu kutoka kwa wanyama wa msitu. Alijifunza kuwa wema hulipwa kwa wema, na kuwa hata kiumbe mdogo anaweza kukuokoa siku moja.

 Tenda wema bila kutarajia malipo, kwa sababu mema hurudi kwa njia usizotarajia.


emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872


0/Post a Comment/Comments