Na, Emakulata Msafiri
hapo zamani sana, kabla ya watu kuishi mjini na magari kujaa barabarani, kulikuwa na kijiji kidogo kilichozungukwa na msitu mkubwa uitwao msitu wa mlimani. katika kijiji hicho aliishi sungura mjanja aitwaye tiko.
tiko alikuwa mcheshi sana, akipenda kucheza na kuwatumbuiza wenzake kwa kuchekesha. lakini pia alikuwa mdadisi kupindukia – kila mara alitaka kujua mambo ya ajabu ajabu, hata yale wanyama wengine walikuwa wanayaogopa.
siku moja, tiko alisikia hadithi kutoka kwa bibi kobe kuwa msituni kuna fimbo ya maajabu iliyowahi kumilikiwa na malkia nondo wa kale, aitwaye nolinda. fimbo hiyo ingeweza kutimiza lolote – iwe ni chakula, nguo, hata kuruka angani.
tiko alishikwa na tamaa na akasema kwa moyo mkunjufu, “nitakwenda kuitafuta fimbo hiyo! nitarudi nikiwa tajiri wa miujiza!”
asubuhi na mapema, tiko alifunga mkoba wake na kuingia msituni. hakuenda mbali sana kabla ya kukutana na kima mzee aliyekuwa anavuta pafu la ndizi juu ya mti.
kima akamuonya:“tiko, msitu huu si wa kawaida. ukikutana na kivuli chenye macho mekundu, usiongee. na fimbo ya nolinda haipatikani kwa tamaa, bali kwa moyo wa kusaidia.”
tiko alicheka,
“mimi ni sungura jasiri! hakuna kivuli wala macho mekundu yanayoweza kuniogopesha.”
kima alitikisa kichwa, “utaona
baada ya masaa kadhaa, tiko alifika kwenye mto ulioitwa mto wa kicheko. kila tone la maji lilikuwa linacheka, na kila aliyejaribu kuvuka alikuwa anaanguka kwa kucheka kupita kiasi.
tiko akajaribu kuvuka, akawa anacheka bila kudhibiti mwili wake. mara akaona nondo mkubwa mweupe, akiwa juu ya jiwe.
nondo akasema:
“kama unahitaji kuvuka huu mto, sema kitu kitakachonifanya nicheke.”
tiko akapiga punzi, akawaza, halafu akasema:
“kwa nini kuku alivuka barabara?”
nondo akashangaa. tiko akamalizia:
“ili aende kununua mayai kutoka kwa bata!”
nondo akacheka sana, mto ukatulia, na tiko akaweza kuvuka.
kukutana na nolinda
baada ya kupita mapango, miiba, na kusikia nyimbo za mizimu, tiko alifika kwenye pango la maajabu, na ndani akamkuta nolinda, malkia wa nondo, akiwa na macho ya kung’aa kama taa.
nolinda akasema:
“kwa nini unataka fimbo yangu, tiko?”
tiko akajibu kwa sauti ya tamaa:
“ili nipate kila ninachotaka – matunda, maparachichi, magari, hata nyumba ya dhahabu!”
nolinda akatikisa kichwa na fimbo yake ikamvutia tiko karibu. akasema:
“fimbo hii huenda tu kwa yule ambaye hutumia nguvu yake kuwasaidia wengine, si kwa tamaa. lakini nitakupa nafasi. ukiweza kutimiza ombi la mnyama yeyote utakayekutana naye sasa hivi, fimbo ni yako.”mtihani wa mwisho: mtoto kobe
tiko alitoka pangoni, akafikiria kwa bidii: “hii ni rahisi, nitatoa chakula au kitu chochote.”
mara akakutana na mtoto kobe, akilia.
tiko akasema, “unahitaji nini, mdogo wangu?”
mtoto kobe akasema kwa sauti ya huzuni:
“sitaki chakula wala zawadi. nataka tu unitembeze hadi kwa mama yangu upande wa pili wa msitu. miguu yangu ni midogo mno, na naogopa peke yangu.”
tiko alisita. safari ilikuwa ndefu, na alihisi ni kupoteza muda. lakini alipomwangalia kobe machoni, alihisi huruma.
bila kusema neno, alimchukua kobe mgongoni, akamsindikiza hadi kwa mama yake, bila kunung’unika.
aliporudi alipokuwa, fimbo ya maajabu ilishakuwa mikononi mwake. nolinda akasema:
“sasa umeelewa – maajabu ya kweli hutoka kwenye moyo wa kusaidia.”
tiko alirudi kijijini na fimbo, lakini hakuitumia kwa mambo ya tamaa. aliitumia kuwasaidia wanyama wagonjwa, kuwasha moto wa jiko wakati wa baridi, na hata kuwasha taa za usiku kwa watoto wa nyani.
wote walimpenda tiko – si kwa sababu ya fimbo, bali kwa sababu alikuwa rafiki wa kweli.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872
Post a Comment