SAFARI YA TOTO NA RAFIKI ZAKE


Na, Emakulata Msafiri

Toto ni mtoto mdogo anayeishi kijijini. Anapenda sana wanyama, hasa marafiki zake wa karibu ambao ni Koko (mbwa mwenye manyoya meupe), Miu (paka mweusi mwenye macho makubwa), na Dede (ndege mdogo wa rangi ya buluu). Kila siku jioni, Toto huenda matembezini na wanyama wake. Wanacheza, kuimba, na kugundua mambo mapya msituni karibu na kijiji chao.

Siku moja ya Jumamosi, waliona kitu kinang’aa msituni. Toto akasema kwa msisimko, “Twende tukaangalie! Huenda ni hazina!” Walikimbia kwa furaha wakipitia njia ya vichaka na nyasi ndefu mpaka walipofika pale. Kumbe ilikuwa ni kioo kilichoanguka kutoka kwa ndege wa angani! Toto alikitazama na kuona sura yake ndani. “Hiki ni cha ajabu sana!” akasema. Marafiki zake walishangaa kuona picha zao ndani ya kioo hicho, wakafurahi sana.


Wakati wakirejea nyumbani, walikutana na nyoka mdogo aliyekwama kwenye matawi. Toto alisita kwanza, lakini Koko akawa anabweka kwa upole, kama kuashiria kuwa nyoka yule hakuwa na madhara. Kwa ujasiri, Toto akasogeza matawi polepole. Miu na Dede walisaidia kwa kutumia miguu yao midogo. Baada ya muda mfupi, nyoka yule alikuwa huru. Aliwashukuru na kusema, “Asanteni kwa moyo wenu mzuri. Siku moja nitawalipa wema huu.”

Toto na rafiki zake walitabasamu. Walijua kuwa walifanya jambo la maana – kusaidia kiumbe kilichohitaji msaada. Walirudi nyumbani na kumwambia mama ya Toto kila kitu kilichotokea. Mama alitabasamu na kusema,


“Mmefanya jambo zuri sana. Ni vyema kuwasaidia walioko katika shida.”

Usiku huo, Toto aliota ndoto nzuri. Aliota kuwa yuko kwenye msitu wa ajabu, na kila mnyama aliyekutana naye alimshukuru kwa kuwa rafiki mwema.

Tuwapende wanyama, kwani nao wana hisia kama sisi na tusaidie walioko kwenye matatizo bila kujali ni nani na pia marafiki wa kweli huungana katika furaha na matatizo.

emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872


0/Post a Comment/Comments