Na, Emakulata Msafiri
Lishe bora ni ulaji wa vyakula vyenye virutubisho muhimu kwa afya ya mwili na akili. Watoto wanaohudhuria shule wanahitaji lishe bora zaidi ili waweze kusoma kwa bidii, kuelewa vizuri masomo, na kukua kwa afya njema.
Watoto wanapoenda shule bila kula chakula cha asubuhi (breakfast), huwa hawana nguvu za kutosha darasani. Akili yao haifanyi kazi vizuri kwa sababu mwili hauna nishati ya kutosha. Chakula cha asubuhi kinapaswa kuwa na wanga, protini, na vitamini, kama vile uji wa mahindi, mkate na mayai, au ndizi na maziwa.
Vyakula vya mchana shuleni pia ni muhimu sana. Watoto wanapaswa kula chakula kilichoandaliwa kwa usafi na kilicho na virutubisho vyote vinavyohitajika. Mfano mzuri ni wali au ugali na maharagwe, samaki au mboga za majani kama mchicha na sukuma wiki. Mboga hutoa vitamini, samaki hutoa protini, na ugali hutoa nguvu.Matunda yanapaswa pia kuwa sehemu ya mlo wa shule. Matunda kama maembe, machungwa, ndizi au papai yanasaidia kuimarisha kinga ya mwili ili mtoto asipate magonjwa kwa urahisi. Watoto wanapaswa kupewa matunda angalau mara moja kila siku shuleni.
Aidha, watoto wanapaswa kuepuka vyakula vya mafuta mengi kama chipsi, mandazi na pipi nyingi. Vyakula hivi si bora kwa afya na vinaweza kusababisha unene kupita kiasi au matatizo ya tumbo. Badala yake, shule zinaweza kuanzisha bustani ndogo za shule ili kupata mboga safi na hata matunda kwa matumizi ya wanafunzi.Lishe bora si jukumu la mzazi peke yake. Walimu, viongozi wa shule na serikali wanapaswa kushirikiana kuhakikisha watoto wanapata chakula bora shuleni. Shule nyingi sasa zimeanzisha programu ya chakula shuleni ili kuwasaidia wanafunzi kula vizuri na kusoma kwa bidii.
Kwa kumalizia, lishe bora ya watoto shuleni ni msingi wa mafanikio yao kitaaluma na kiafya. Mtoto mwenye lishe bora hukua vizuri, anakuwa na nguvu, akili timamu na uwezo mzuri wa kujifunza. Tuimarishe lishe ya watoto wetu ili tuijenge jamii yenye afya na mafanikio.emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872
Post a Comment